Sunday, June 26, 2011

AZALILISHWA KWA KUDUNGWA SINDANO SEHEMU YA HAJA KUBWA

JESHI la Polisi mkoani Rukwa
linamtafuta mwanamke mmoja
mkazi wa mtaa wa Lwiche
Kitongoji cha Mazwi katika
Manispaa ya Sumbawanga kwa
tuhuma ya kumchoma sindano
iliyowekwa maji ya moto mtoto
mwenye umri wa miaka sita
kwenye sehemu yake ya haja
kubwa kwa madai kuwa ni
kikojozi.
Mwanamke huyo aitwaye Severia
Mpepo anatuhumiwa kumfanyia
unyama huo mtoto huyo na
kumsababishia maumivu makali
juzi majira ya saa moja asubuhi.
Kitendo hicho kisicho kawaida
kilisababisha mtoto huyo ambaye
ni wa kiume kupiga kelele za
kuomba msaada kutoka kwa
majirani kabla ya kuzimia na
kukimbizwa na wasamaria katika
Hospitali ya Mkoa wa Rukwa kwa
ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa majirani wa
mtoto huyo ambao hawakutaka
kutajwa majina yao walisema
kuwa tukio la kuunguzwa
linafuatia mateso mfululizo
aliyokuwa akiyapata kutoka kwa
mama mlezi wake, Severia
ambaye amekuwa akimlea kwa
kipindi cha miezi sita tangu
kufariki kwa mama mzazi wa
mtoto huyo.
Majirani hao walisema mtoto
huyo aliletwa kwa mlezi huyo na
babake mzazi anayefahamika
kwa jina la Peter Matalanganya
kufuatia ushauri wa rafiki yake
ambaye ndiye mume wa Severia
aliyemshauri kuwa ampeleke
kwake ili apate kumlea baada ya
mkewe kufariki dunia.
“Tunasikia kuwa huyu mtoto
aliletwa hapa na babake miezi
sita iliyopita baada ya mamake
kufariki, lakini kuanzia alipofika
huyu mwanamke amekuwa
akimtesa sana mara amnyime
chakula, mara amchape na juzi
ndio kahitimisha kwa kumfanyia
huu unyama wa kumwunguza
katika sehemu yake ya haja
kubwa, kwa kweli huyu mama
hafai na ni muuaji mkubwa,“
walisema majirani hao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Saduni
Kabuma alikiri kumpokea mtoto
huyo hospitalini hapo na
kupatiwa tiba ambapo katika
uchunguzi alionekana kuwa
ameunguzwa katika sehemu za
haja kubwa na maji hayo kiasi
cha kumsababishia
malengelenge.
Dk. Kabuma alisema kuwa taarifa
alizopata kutoka kwa ndugu wa
karibu waliomfikisha hospitalini
hapo zimedai mama mlezi wa
mtoto huyo alichukua uamuzi
huo wa kinyama kwa kuwa
kijana ni kikojozi wa kupindukia.
Naye Daktari aliyempokea mtoto
na kumpatia huduma ya
matibabu katika kitengo
wagonjwa wa nje, Dk. Revocatus
Kasoni alisema kuwa hali ya
mtoto huyo inaendelea vizuri na
kuongeza kuwa bado yupo
katika uchunguzi wa kitabibu
zaidi.
Alipoulizwa na waandishi wa
habari waliofika nyumbani
kwake kutaka kufahamu undani
wa tukio hilo alikiri kutenda
unyama huo, lakini alisema
hakutenda kwa makusudi bali
alikuwa anampatia mtoto huyo
tiba ya ugonjwa wa tumbo kwa
kumpiga bomba.
Kamanda wa Polisi mkoani
Rukwa Isuto Mantage
alipoulizwa kuhusu tukio hilo
alisema kuwa mama huyo bado
hajakamatwa na Jeshi hilo
linaendelea kumsaka mama huyo
ili sheria ichukue mkono wake
iwapo ikibainika kuwa alitenda
uovu huo.
....

No comments:

Post a Comment