MWALIMU raia wa Uganda, Paul
Lubega (27) anayetuhumiwa
kumuiba mwanafunzi Ibrahim
Laurence (7) wa Shule ya Msingi
ya Mchepuo wa Kiingereza ya
Samaria ya mjini Moshi,
amesisitiza kutaka kulipwa Sh
milioni 3.5 ili amrejeshe,
vinginevyo atamuua mtoto huyo.
Kwa mujibu wa babu wa
mwanafunzi huyo, Moses
Laurence, mtuhumiwa huyo
alipiga simu tena Jumapili usiku
akisisitiza azma yake ya kulipwa
fedha hizo.
“Huyu mwalimu amempigia simu
mke wangu, Elinaike Moses
akiulizia kama fedha hizo
zimepatikana. Lakini pia alisema
hataki kuwasiliana na simu ya
zamani, bali wanunue namba
mpya kisha ndipo wamtafute,”
alisema Mzee Laurence jana
alipozungumza na gazeti hili.
Laurence alisema, mtuhumiwa
huyo ametoa muda hadi kufikia
Julai 21, mwaka huu awe
amepewa fedha hizo, vinginevyo
atakuwa amemuua mtoto huyo
na kurejesha maiti katika familia
hiyo.
“Sasa sisi tumepata wakati
mgumu, maana mama (bibi)
anatumia mtandao ambao
mtuhumiwa ndiyo anataka uwe
wa kuwasiliana naye (Airtel)
….ametoa muda hadi Alhamisi
awe amepewa hizo fedha
vinginevyo tutapokea maiti,”
alisema babu huyo.
Alisema, kutokana na taarifa hiyo,
mkewe alikwenda kutoa taarifa
Kituo cha Polisi Majengo kwa ajili
ya kuomba msaada zaidi, lakini
hadi kufikia jana mchana
hapakuwa na taarifa za
kupatikana kwa mtoto au
mtuhumiwa huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Meneja
wa Shule ya Samaria, Batholomeo
Bigendako alisema, mtuhumiwa
huyo hakuwa mwalimu wa
kudumu shuleni hapo, bali
aliomba kazi ya kufundisha kwa
muda Kiswahili.
Tukio la kuibwa kwa mtoto huyo
lilitokea Julai 14, saa 9:30 alasiri
shuleni hapo baada ya shule hiyo
kufungwa kwa ajili ya likizo.
Inadaiwa mtuhumiwa ambaye
pia ni mwanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Makerere nchini
Uganda akisomea taaluma ya
Ualimu, aliondoka na mtoto huyo
na haikujulikana alipokwenda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma,
alisema hadi sasa mtoto huyo
hajapatikana ingawa jeshi hilo
linafanya juhudi kubwa za
kumsaka.
Akielezea mazingira ya tukio,
alisema Julai 15, Laurence
alipigiwa simu namba
+254739665740 na kumuuliza
kama anamfahamu mtoto
Ibrahimu, lakini alipoulizwa kama
yupo na mtoto huyo hakujibu
tena na alikata simu na
hakupokea tena hata
alipopigiwa.
Kamanda Mwakyoma alisema,
Julai 16, saa 12 jioni, familia hiyo
ilipokea simu nyingine yenye
namba 025675361094 na mtu
anayedhaniwa ni mtuhumiwa
akitaka alipwe Sh milioni 3.5.
Kamanda huyo ameomba mtu ye
yote mwenye taarifa juu ya
mhalifu huyo atoe taarifa kupitia
namba 0754 293349, 0787
550996 au atume ujumbe
kupitia namba 0767 750175 na
atazawadiwa.
No comments:
Post a Comment