Wednesday, July 13, 2011

SITA;''wapinzani ni wanafiki''

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, amesema
mambo mengi ya wapinzani ni
ya kinafiki na wamekuwa
wakiibeza Serikali kwa kauli
nyepesi nyepesi.
Sitta alitoa kauli hiyo jana
bungeni mjini Dodoma
alipokuwa akijaribu kutuliza
Bunge lililokuwa limechafuka
baada ya Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila (NCCR-
Mageuzi), kudai kuwa Serikali
iliyoko madarakani ni legelege na
imeshindwa kukusanya kodi.
"Nawasihi wenzangu hasa wa
CCM, hawa wapinzani hii
(kupinga mambo) ndiyo kazi yao,
wanabeza kila tunachofanya kwa
lugha nyepesi nyepesi na mambo
mengi wanayozungumza ni
unafikinafiki hivi, sisi tuwaachie
wananchi wawahukumu.
Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya
wabunge hasa wa upande wa
upinzani kusimama na kuomba
mwongozo wa Mwenyekiti na
wengine wakizomeana, huku
Sitta ambaye ni Kaimu Kiongozi
wa Shughuli za Serikali Bungeni,
akiwa amesimama akiomba
kuendelea.
"Subirini nitoe mfano ...
wanazungumza posho za vikaoni
ni kuibia wananchi na baadhi
yao wamekuwa wabunge kwa
miaka mitano iliyopita na
walikuwa wakizichukua, kama
kweli ndivyo hivyo, basi
warudishe," alisema Sitta.
Kauli hiyo ilisababisha wabunge
zaidi, karibu 10 wakiwamo wa
CCM kusimama kuomba
Mwongozo wa Mwenyekiti, lakini
Mwenyekiti Jenista Mhagama
akaahirisha shughuli za Bunge
kwa mapumziko ya mchana, kwa
kuwa muda ulikuwa umefika,
huku akiwaacha wabunge
wakipiga kelele za kuomba
Mwongozo.
Kabla ya kuibuka tafrani hiyo,
Kafulila aliyekuwa akichangia
hotuba ya Makadirio ya Matumizi
ya Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, alisema tangu Uhuru moja
ya maadui waliopigwa vita ni
maradhi; lakini akashangaa
bajeti ya Afya ni ndogo na
kuongeza kuwa inatokana na
Serikali legelege kushindwa
kukusanya mapato.
"Miaka 50 ya Uhuru asilimia 90
ya bajeti ya maendeleo ya afya
inategemea fedha za nje, tatizo
hamkusanyi kodi na Nyerere
(Baba wa Taifa) alisema Serikali
legelege inashindwa kukusanya
kodi," alisema Kafulila.
Kauli hiyo ilipingwa na Mbunge
wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala
(CCM) aliyesema Kafulila alitumia
neno la kuudhi kwa kuiita
Serikali ya CCM legelege.
Dk. Kigwangala alifafanua kuwa
Kafulila hakuwa na taarifa sahihi,
kwa kuwa katika miaka mitatu
iliyopita, Serikali ilikuwa
ikikusanya karibu Sh bilioni 200,
lakini mpaka mwaka huu,
makusanyo yaliongezeka na
kufikia karibu Sh bilioni 400.
Baada ya ufafanuzi huo,
Mwenyekiti wa Bunge, Mhagama
alimtaka Kafulila kufuta usemi,
lakini mbunge huyo alipinga
akisema ni kauli ya Baba wa
Taifa, ambaye kila mtu
anamuenzi bila kujali anatoka
chama gani.
"Tunapoteza muda kujadili suala
ambalo liko wazi, mwaka
2005/06 Serikali ilikuwa
ikikusanya wastani wa Sh bilioni
260 lakini dola moja ilikuwa
sawa na Sh 1,000.
"Leo mnakusanya karibu Sh
bilioni 400 kwa mwezi, dola
moja ni Sh 1,600 ni hesabu
rahisi, hakuna kilichoongezeka ...
sifuti usemi, niko tayari kufia
ukweli huu," alisema Kafulila na
kusababisha Sitta kuamka na
kuwaita wapinzani wanafiki
huku akiwataka CCM
kuwavumilia.
Hata hivyo, Mwalimu Nyerere
alisema chama legelege huzaa
Serikali legelege na pia aliwahi
kusema "Serikali corrupt
(inayokula rushwa) hushindwa
kukusanya kodi," na si Serikali
legelege hushindwa kukusanya
kodi.
Awali, kabla ya tafrani hiyo,
Kafulila alimtaka Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji
Mponda, ikibidi ajiuzulu kuliko
kukubali kuwasilisha bajeti ya
fedha ndogo bungeni huku
ikitegemea fedha nyingi za
wahisani.
Alisema hiyo inatokana na
wabunge na familia zao kuwa na
uwezo wa kutibiwa sehemu
yoyote ndani na nje ya nchi,
ndiyo maana hawawekezi katika
hospitali za vijijini.
Wakati akisema hayo, mmoja wa
wabunge ambaye hakufahamika
lakini mwanamke, aliwasha
kipaza sauti akasema: "Pamoja
na wewe (Kafulila) na Mbunge
wa Mpanda Mjini Chadema (Said
Arfi ambaye alilazwa India hivi
karibuni)."
Hata hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uwekezaji na
Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu,
alisimama na kupinga kauli ya
Kafulila, akisema: "Hili ni Bunge
Tukufu, tuzungumze kwa
heshima."
Mbunge mwingine mwanamume
akawasha kipaza sauti na kuhoji:
"Nani ana heshima?" Nagu
akaendelea kufafanua kuwa
mwanawe ni daktari katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
ambayo ni ya Serikali na hata
baba yake mzazi alilazwa katika
hospitali ya Katesh ambayo ni ya
vijijini.
Hata hivyo, sauti ile ya kiume
iliendelea kumkatisha Nagu na
safari hii Mbunge huyo alisema,
"so what(kwa hiyo?"
Kutokana na kauli hizo za
kukatishana, Mhagama alisimama
na kusema ameisikiliza sauti ya
mmoja wa wabunge wanaotoa
kauli hizo za kejeli huku
akimkatisha waziri aliyekuwa
akizungumza na kubaini kuwa
sauti hiyo inafanana na ya
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia
Wenje (Chadema).
Alionya kuwa wanachofanya
wabunge kuwasha vipaza sauti
holela ili kuzuia hoja za wenzao
kusikika au kuwakatiza, ni
kinyume na Kanuni za Bunge na
akifuatilia anaweza kuwabaini na
kuwachukulia hatua.

No comments:

Post a Comment