Monday, August 15, 2011

MAFUTA BEI JUU KWA 5%

BEI ya bidhaa ya petroli
imepanda tena kwa zaidi ya Sh
100 kwa lita kuanzia Jumatatu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
ya Nishati na Maji (Ewura)
imetangaza Jumapili.
Kwa tangazo hilo la Ewura, katika
Jiji la Dar es Salaam lita ya petroli
imepanda hadi kufikia Sh 2,114
ambayo ni bei kikomo kutoka Sh
2,004 zilizotangazwa na Ewura
Agosti 3, mwaka huu ambazo
hata hivyo ziligomewa na
wafanyabiashara.
Dizeli kwa bei ya rejareja sasa
itauzwa Sh 2,031 kutoka Sh
1,911 huku mafuta ya taa
yatauzwa kwa Sh 2,005. Kwa
upande wa bei za jumla petroli
itauzwa kwa Sh 2,046.62, dizeli
itauzwa kwa Sh 1,963.81 na
mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh
1,937.90.
Wiki mbili zilizopita, Ewura
ilitangaza bei hizo mpya ambazo
ziligomewa na wafanyabiashara
wa mafuta hadi Serikali ikatishia
kuchukua hatua za kisheria dhidi
yao ndipo baadhi yao
wakalegeza msimamo.
Hata hivyo, Kampuni ya BP
Tanzania iliendelea na msimamo
wa kutouza mafuta kwa bei hiyo
ya Serikali na kwa ukaidi huo
tayari kampuni hiyo imefungiwa
na Ewura kutojihusisha na
biashara ya petroli, dizeli na
mafuta ya taa kwa miezi mitatu.
Hatua hii ya Ewura kupandisha
bei tena ya mafuta ni wazi kuwa
itazua manung’uniko kwa
wananchi ambao walitarajia
kuwa ile ahadi ya Serikali iliyoitoa
wakati wa bajeti ya kushusha bei
za bidhaa hiyo ingedumu kwa
muda mrefu.
Meneja Biashara ya Petroli wa
Ewura, Godwin Samwel alitetea
uamuzi wa kupandisha bei ya
mafuta kuwa umetokana na
kushuka kwa thamani ya Shilingi
dhidi ya Dola ya Marekani pamoja
na kupanda kwa kwa bei ya
mafuta katika soko la dunia.
Samwel alisema viwango vya bei
zilizotumika katika soko la dunia
zimepanda kwa wastani wa
asilimia 5.42 na thamani ya
Shilingi ya Tanzania imeshuka
kwa shilingi 47.12 kwa Dola
moja ya Marekani.
Ewura pia imezidi kujitetea kuwa
kanuni mpya ya kukokotoa bei za
bidhaa hiyo bado inafanya
mafuta kuuzwa kwa bei ya chini
ukilinganisha na kanuni ya
zamani. Samwel alitoa mfano
kuwa iwapo Ewura ingetumia
kanuni ya zamani ya kukokotoa
bei mpya, petroli ingeuzwa kwa
Sh 2,298.33, dizeli ingeuzwa Sh
2,213.36 wakati mafuta ya taa
yangeuzwa kwa Sh 2,188.89.
“Bei za rejareja na za jumla
zingepanda zaidi endapo
furmula ya zamani ingeendelea
kutumika,” alisema Meneja
Biashara ya Petroli wa Ewura.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa
Sheria ya Mafuta ya Ewura ya
mwaka 2008, bei za bidhaa ya
petroli zitaendelea kupangwa na
soko na akaongeza kuwa
mamlaka yake itaendelea
kuhamasisha ushindani kwa
kutoa taarifa za bei za bidhaa za
mafuta.
Hata hivyo, Samwel alitoa
matumaini kwa Watanzania
kuwa kuna uwezekano mkubwa
baada ya wiki mbili bidhaa ya
petroli ikapungua bei kutokana
na bei katika soko la dunia
kuanza kushuka.
“Bei itashuka iwapo Shilingi
haitaporomoka zaidi, ila
ikiendelea kuporomoka bei
haitashuka sana,” alisema ofisa
huyo wa Ewura. Akielezea hali ya
biashara ya mafuta kwenye soko
la ndani, alisema upatikanaji wa
mafuta unaendelea vizuri kwani
Ijumaa jumla ya lita milioni 9.5
zimeingizwa kwenye soko la
ndani na juzi Jumamosi lita
milioni 4.9 za bidhaa hizo
ziliingizwa kwenye soko.
Alisema meli za mafuta
zinaendelea kuingia nchini na
zingine ziko bahari zikisubiri
kupakua shehena hiyo. “Hivyo
nawahakikishia kuwa
upatikanaji wa mafuta
utaendelea kuwa mzuri,” alisema.
Kuhusu baadhi ya vituo vya
Kampuni ya Total na Orxy
kuendelea kutotoa huduma kwa
wananchi, Ewura imeahidi kutoa
tamko leo.

.
[chanzo Habari Leo]

No comments:

Post a Comment