Mjumbe maalum wa Umoja wa
Mataifa kwa Somalia Balozi
Augustine Mahiga, anasema
kundi la wanamgambo wa al-
Shabaab lenye ushirika na
mtandao wa kigaidi wa al-Qaida
limeondoka Somalia, lakini
anatahadharisha kuwa huenda
kukaibuka makundi ya kujazia
pengo lililoachwa na al-Shabaab.
Mahojiano na Balozi Mahiga
Akizungumza na Sauti ya
Amerika leo Alhamis, akiwa mjini
Kampala ambapo alitazamiwa
kukutana na Rais Yoweri
Museveni, Balozi Mahiga alisema
ameliomba Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa pamoja na
Umoja wa Afrika kuongeza
juhudi na mchango wao wa
kijeshi kusaidia serikali ya
Somalia ili iweze kujenga mfumo
thabiti wa utawala na taasisi za
kutegemewa kwa raia wa
Somalia.
Aidha Balozi Mahiga, alisema
mkusanyiko wa maswala kadha
huenda ulipelekea kuvunjwa
nguvu kwa kundi hilo la al-
Shabaab, ikiwemo ukosefu wa
fedha, kukosa uongozi thabiti na
hata matatizo ya njaa na ukame.
Lakini alisitiza kuwa kulikuwa na
mapambano makali baina ya al-
Shabaab na vikosi vya serikali ya
Somalia vikisaidiwa na majeshi
ya Umoja wa Afrika-AMISOM kwa
siku 10 hivi, kabla ya kundi hilo
kusalim amri.
Kuhusu ukame na njaa
iliyokumba Somalia, Balozi
Mahiga alisema alianza kuonya
juu ya uwezekano wa kuibuka
janga kubwa la njaa tangu
mwezi Oktoba mwaka jana, kwa
kutoa taarifa kwa katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa. Anasema
endapo jamii ya kimataifa
ingeliingilia kati tangu wakati
huo, maafa na picha za
kuhuzunisha zinazoshuhudiwa
na dunia nzima kuhusu njaa
nchini Somalia yangeepukika.
Mjumbe huyo maalum wa Umoja
wa Mataifa kwa Somalia pia,
alisema yupo tayari kuhamia
Mogadishu, na anahimiza jamii
ya kimataifa ichangie kuhamishia
makao ya ofisi yake mjini humo
badala ya Nairobi ili kuweza
kutoa huduma zaidi na kwa
wakati ufaao, kusaidia kuleta
uthabiti wa kiutawala nchini
Somalia.
No comments:
Post a Comment