Thursday, June 28, 2012
Dr.Shein kutetea muungano kinyume namatakwa ya wananchi ?
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema
ataendelea kuutetea Muungano na hakuna
atakaemlaghai wala kumchezea katika uongozi
wake. Kauli hiyo ameitowa jana katika mkutano wa
Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Bwawani mjini
Unguja. Dk Shein amesema kwamba yeye ndie rais wa
Zanzibar na ndie mwenye mamlaka na
hatomuogopa mtu wala kusita kuwachukulia
hatua kwa wale wote ambao watakwenda
kinyume na matakwa ya kikatiba. Alisema kuwa dhamana ya nchi hii pamoja na ile ya
Jamhuri ya Muungano imo mikononi mwao kati
yake na Rais Jakaya Kikwete na ndio maana
wakawa wanashirikiana na kushauriana kwa yale
yote ambayo yana maslahi na nchi. “katika kuiongoza Zanzibar mimi ndie rais
simuogopi mtu yeyote”, alisema kwa kujiamini Dk
Shein. Dk Shein alisema Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia
inayotoa uhuru wa maoni kwa kila mtu, lakini kwa
upande wake pia yeyé ndio mwenye dhamana
kubwa ya kuendesha nchi kwa mujibu wa katiba
iliyopo. “Mimi ndio rais siogopi mtu katika
kuendesha nchi, siko tayari kuirudisha nchi katika misukosuko na kuirejesha Zanzibar kule ilipotoka
wakati iko katika hali ya amani hivi sasa,” alisema
katika mkutano huo. Hata hivyo alisema kuwa Muungano upo na
utaendelea kuwepo na kwani yeye ndiye rais
ambaye anatokana na chama cha mapinduzi na pia
ameingia madarakani chini ya ilani ya chama chake
hivyo lazima afuate ilani ya chama chake ambapo
alisema changamoto zilizomo zinahitaji kujadiliwa ili kuweza kuziondoa na sio kuvunja muungano. “Hakuna mtu asiyejua kuwa kuna kero za
Muungano hivyo ni vizuri tukajitokeza kwa wingi
katika kutoa maoni yetu juu ya katiba na sio kukaa
pembeni yanazungumzwa mengi kuhusu mimi
lakini yote nimeyapokea kwa kuwa ukubwa ni
jaa”, alisema Dk Shein bila ya kutaja jina lakini alikuwa akijibu hoja zilizokuwa zimeibuka kuwa
hana uwezo wa kuchukua maamuzi magumu
katika suala la uongozi. Aliwaeleza wastaafu hao kwamba Muungano una
kero, zinazojadiliwa na ndio maana njia nyingi,
ikiwemo ya mawasiliano baina ya Rais wa Zanzibar
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zimeanzishwa ili kuzitafutia ufumbuzi ambapo
alisema njia hizo zitaendelea kutatua mambo ya muungano. Aidha Dk Shein alisema kazi hiyo anaifanya kwa
umakini ili kuhakikisha kuwa Muungano upo na
unazidi kuwepo na kwamba wasioutaka wasubiri
tume ikija ndio watoe maoni yao na sio kuanza
kutoa maoni hivi sasa kabla ya wakati hufika. “Hakuna asiyejua katika Muungano kuna kero,…
wananchi wazijadili kupitia tume ya mabadiliko ya
katiba, na kwa nini tunaanza kusema sema…
subirini tume mkatoe maoni yenu” alisema. Katika hatua nyengine Dk Shein alisema kwa
sababu hiyo anaagiza kutokufanyika kwa
maandamano ya aina yoyote kuhusiana na suala
hilo na kuwataka wazanzibari kutoshiriki hadi pale
wanaotaka kufanya hivyo wanaporuhusiwa
kuandamana na jeshi la polisi kwa kufuata taratibu za kisheria. “Naagiza maandamano yasifanyike,…
wakiruhusiwa kufanya basi msiende kushiriki,”
alisisitiza Dk Dk Shein alikuwa akizungumza na
zaidi ya watu 500, waliohudhuria katika mkutano
huo, ambao ni wastaafu wa taasisi za Muungano
waliopo Zanzibar. Katika waliohudhuria katika mkutano huo ni taasisi
mbali mbali pamoja na Bunge, Ulinzi na Uslama,
Mambo ya Nje, Mamlaka ya hali ya hewa (TMA),
Mamlaka ya Kodi na mapato (TRA), Mamlaka ya
Usafiri wa Anga (TCAA), Idara ya Uhamiaji, Shirika la
Posta na Simu, na taasisi za masuala ya elimu na ufundi. Sambamba na hayo aliwataka vijana kuthami ni
jitihada, michango na maelekezo ya wastaafu kwa
kutambua kuwa uzoefu wao katika maisha ni
sehemu muhimu kwa maendeleo yao. “Sote hatuna budi kuelewa kuwa iko siku
tutakuwa wastaafu hivyo ni muhimu kujitayarisha
hasa kwa kujenga tabia ya kujiwekea akiba na
matayarisho mengine ya lazima kwa maisha ya
wastaafu”, alisema. Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa
jumuiya hiyo , Mohamed Ali Maalim, alisema
miongoni mwa majukumu ya jumuiya hiyo ni
kudumisha Muungano kwa sababhu unalinda
maslahi ya wastaafu wote nchini. Katika risala yao wastaafu hao wamesema kwamba
wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ndani ya
Jumuiya yao ikiwemo uwezo mdogo wa
uendeshaji na usimamizi wa ofisi ikiwemo ukosefu
wa ofisi ya kutosheleza mahitaji. Katibu mkuu wa Jumuiya hiyo Rashid Ali alitaja
changamoto nyengine ni kukosekana kwa
wataalamu na waratibu wa kusimamia utekelezaji
wa mipango ya Jumuiya, ukosefu wa vitendea kazi,
ukkatika kutekeleza malengo yao. Jumuiya ya wastaafu Zanzibar imeanzishwa mwaka
2009 ina wanachama 537 ambapo 486 kati ya hao
ni wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Source mzalendo.net
No comments:
Post a Comment