Sunday, August 12, 2012
MJUSI ALIYEPELEKWA UJERUMANI KUREJESHWA NCHINI
SERIKALI ina mpango wa kumrudisha nchini
mjusi maarufu aina ya Dinosaur
aliyechukuliwa mkoani Lindi zaidi ya miaka
100 iliyopita na kupelekwa Ujerumani
anakokadiriwa kuiingizia nchi hiyo zaidi ya
Dola za Marekani bilioni tatu kwa mwaka,
sawa na karibu Sh trilioni tano.
Hayo yalisemwa bungeni juzi na Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
alipozungumzia mikakati ya serikali katika
kukuza utalii nchini. Nyalandu alisema
Serikali itazungumza na Serikali ya
Ujerumani juu ya suala hilo na kwamba,
kama atarudishwa, atapelekwa mkoani
Lindi.
Aidha, alisema kama hilo litashindikana
wataangalia pia uwezekano wa kupata
asilimia fulani ya fedha inayotokana na
watalii wanaomiminika kumuona mjusi
huyo.
“Katika mambo ya Kale, kuna hili la Mjusi
wetu maarufu kama Dinasour ambaye
taarifa tulizonazo anaipatia Ujerumani dola
bilioni tatu kwa mwaka… huyu alichukuliwa
Lindi na wakoloni wa Ujerumani
akapelekwa iliyokuwa Berlin Mashariki…
tunataka tumrudishe nchini, tutazungumza
na Ujerumani… “Lakini niwahakikishie
wabunge na Watanzania, tutawashirikisha
wadau ili tujue sera na mtazamo wetu kama
taifa kuona tutakavyoamua kuzungumza na
Ujerumani tuamue kuomba mjusi wetu
arudi tumweke Lindi au abaki huko huko,
lakini tugawane mapato,” alisema.
Masalia ya mifupa ya mjusi huyo,
yalipatikana mwaka 1912 huko Tendaguru,
Kata ya Mipango katika Jimbo la Mchinga,
mkoani Lindi. Amehifadhiwa katika
Makumbusho ya Humbolt huko Ujerumani.
Nyalandu alikiri kuwapo kwa changamoto
nyingi katika kukuza utalii, lakini Serikali
imejipanga kufanya kazi kwa kasi ili
kuhakikisha yanafanyika mapinduzi
makubwa katika sekta ya utalii ili
ulinufaishe taifa.
Alisema “Hali ya utalii nchini hairidhishi na
wizara yangu imeazimia kufanya
mabadiliko makubwa. Nchi yetu inapata
watalii wachache tofauti na fursa
tulizonazo. Dhamira ya Serikali ni kuona nchi
inapata watalii milioni mbili kwa mwaka
ifikapo mwaka 2015. Kwa sasa, watalii
hawafiki milioni moja kwa mwaka.”
Alisema mikakati hiyo itakwenda sambamba
na kuongeza kasi ya ujenzi wa hoteli na
nyumba za kulala wageni ili kuwa na
uhakika wageni watakaokuja nchini
hawakosi makazi.
Nyalandu alisema mikakati pia inafanywa
kuboresha mazingira ya viwanja vya
ndege, akitolea mfano Uwanja wa Ndege
wa Mwanza utapandishwa hadhi na
mpango wa kuufanya kuwa wa kimataifa
zaidi, utabadilishwa jina na kuitwa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti.
No comments:
Post a Comment