Sunday, September 29, 2013
Mwananchi na Mtanzania Yafungiwa
SERIKALI imeyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kutokana na kuandika habari na makala za uchochezi. Gazeti la Mwananchi linalomilikiwa na Kampuni ya Mwananchi Communications limefungiwa kwa muda wa siku 14, wakati Mtanzania linalomilikiwa na Kampuni ya New Habari 2006, likifungiwa kwa miezi mitatu, kutokana na kutaka kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
Akitoa tamko hilo la serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene alisema kuwa serikali imefikia hatua ya kuyafungia magazeti hayo kutokana na habari za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani na vyombo vya dola na kuhatarisha amani na mshikamano uliopo.
Akizungumzia kuhusu kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi, alisema gazeti hilo limefungiwa muda wa siku 14 ambapo adhabu hiyo ilitangazwa kwa tangazo la serikali namba 333 la Septemba 27, mwaka huu.
Alisema gazeti hilo hivi karibuni lilichapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani, ambapo alitolea mfano gazeti la Julai 17, mwaka huu toleo namba 4774 ilichapisha habari iliyokuwa ikisema "Mishahara Mipya Serikalini 2013" ambao ulikuwa ni waraka uliozuiwa kwa matumizi ya vyombo vya habari kwa kuwa ulikuwa ni wa siri na haukupaswa kuchapishwa magazetini.
"Aidha, katika toleo la Jumamosi, Agosti 17, mwaka huu lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “Waislamu Wasali Chini ya Ulinzi Mkali" habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira.
Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu, jambo ambalo halikuwa la ukweli," alisema Mwambene.
Alisema katika siku hiyo polisi haikupeleka mbwa katika maeneo ya misikiti kama gazeti hilo lilivyoripoti, kwani serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Aliongeza kuwa gazeti hilo kwa kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya Kiislamu, kwani mbwa ni najisi hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada.
Akizungumzia gazeti la Mtanzania, alisema limefungiwa kuchapishwa kwa siku 90 (miezi mitatu) kwa kuchapisha habari zenye uchochezi, ambapo alisema gazeti hilo limeonywa mara nyingi kwa kutakiwa kurekebisha mtindo wake wa uandishi na lizingatie maadili, Sheria na Kanuni za fani ya Habari.
"Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano katika toleo na. 7262 la Machi, mwaka huu, liliandika habari yenye kichwa kisemacho; “Urais wa Damu”, na Juni 12 katika toleo namba 7344 lilichapisha makala isemayo “Mapinduzi Hayaepukiki”.
"Aidha, siku ya Jumatano, Septemba 18, mwaka huu katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha kichwa cha habari kisemacho; “Serikali yanuka Damu” taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizounganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.
Katika habari hiyo, gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na waathirika walioumizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliovamiwa na kujeruhiwa vibaya," aliongeza Mwambene.
Gazeti hilo pia limeishutumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi nchini. Alisema kwa ujumla habari hiyo ni ya kichochezi, ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama wavione kuwa haviwasaidii.
“Kutokana na makosa yaliyotajwa hapo juu serikali imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku 90 kwa Tangazo la Serikali Namba 332 la Septemba 27, mwaka huu”.
"Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili ya taaluma ya uandishi wa habari. Vile vile inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya taifa letu, kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu," alisema.
Aliongeza kuwa serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo ya kuvifungia.
"Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani
No comments:
Post a Comment