Wednesday, September 25, 2013
Tanzania yachunguza vitisho vya al-Shabaab
Vyombo vya usalama nchini Tanzania vinachunguza tuhuma za kuwepo kwa vitisho vya al-Shabaab ambazo zimejitokeza kwenye tovuti na mitandao ya kijamii katika siku chache zilizopita.
"Siwezi kusema ni aina gani ya uchunguzi tunaoufanya kwa sababu ni siri yetu, lakini tunajua juu ya kuwepo kwa vitisho hivyo na tayari tumeanzisha uchunguzi," Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu (tarehe 23 Septemba).
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima, aliiambia Sabahi siku ya Jumanne kwamba Tanzania imejitayarisha vya kutosha na iko kwenye tahadhari.
"Ni kweli tumepokea taarifa hizo kuhusiana na vitisho kutoka makundi haya ya kigaidi, lakini kama serikali tumejitayarisha," alisema. "Hatuwaogopi al-Qaeda wala al-Shabaab. Kama serikali, tuko tayari kuwalinda watu wetu na musiwe na hofu. Serikali ipo na imejitayarisha vyema kwa chochote kitakachotokea."
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Meja Eric Komba, pia alisema siku ya Jumatatu kwamba jeshi hilo lilikuwa "kwenye hali ya tahadhari kuyalinda maisha ya Watanzania" kama lolote litatokea.
Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Senso, aliwatolea wito raia kuripoti jambo lolote wanalolitilia wasiwasi.
"Tumeanzisha operesheni ya kujenga uelewa wa masuala ya usalama kwenye mipaka ambayo wageni wenye nia mbaya hupitia. Wananchi wanapaswa kujua wafanye nini na wakati gani," alisema Senso.
No comments:
Post a Comment