SIRI ya mafanikio ya Padri feki, Josephat Asenga, aliyekamatwa mkoani Morogoro, katika kuongoza Misa ya Kanisa Katoliki kwa kufuata taratibu zote maalumu bila kutiliwa shaka, imebainika.
Asenga aliyetumia vitambulisho feki, alipojitambulisha kwa uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria Madeko mkoani Morogoro, alipopewa fursa ya kuongoza Misa, alitekeleza wajibu huo wa kipadri bila kuacha shaka.
*Alivyojitambulisha
Akizungumza na gazeti hili jana, kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki (jina limehifadhiwa), alithibitisha kuwa Asenga alipofika Parokiani hapo kati ya Mei na Juni mwaka jana, hakutiliwa shaka hata kidogo kuwa si Padri.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Asenga alifika kanisani hapo akiwa amevaa mavazi ya kipadri na kujitambulisha kuwa yupo nchini kwa mapumziko, akitokea nchini Marekani, alikodai ndipo anakofanyia shughuli zake za upadri katika Jimbo Kuu la New York.
Mbali na kuvalia mavazi ya kipadri, Asenga pia alionesha kitambulisho na kusababisha uongozi uamini kuwa ni Padri na kumpa makaribisho ya Padri mwenzao.
“Alipoonesha kitambulisho tulimwamini na jinsi alivyokuja na mavazi ya upadri na muonekano wake alionao, haikuwa rahisi kumtilia shaka,” alisema kiongozi huyo.
*Kuongoza Misa
Baada ya kupata makaribisho ya kipadri, Asenga kwa mujibu wa kiongozi huyo, aliomba apangiwe zamu ya kuongoza misa ya Jumapili iliyofuata na kukubaliwa. Kiongozi huyo alithibitisha kuwa Asenga aliongoza vyema misa hiyo, kwa kufuata taratibu zote za kanisa hilo kama zinavyofuatwa na mapadri wengine.
Taratibu Kwa kawaida Misa katika Kanisa la Katoliki, huanzia Sakestia, sehemu ambayo mapadri na waministranti, ambao ni wasaidizi wao, huvaa majoho na kusali kabla ya kuingia kanisani wakisindikizwa na nyimbo.
Baada ya kuingia madhabahuni, Padri hubusu madhabahu kabla ya kualika waumini katika Misa. Mualiko huo hufuatiwa na maelezo kidogo na kuanza Ibada ya Kitubio, ambayo waumini hutubu dhambi zao na kujiweka tayari kusikiliza neno la Mungu.
Ibada ya kusomwa neno, kwa kawaida masomo matatu kutoka vitabu vya Agano la Kale na Jipya katika kitabu cha Bibilia Takatifu, Padri huanza kutoa mahubiri.
Mahubiri yakiisha, Misa huendelea kwa sadaka na baadaye, Padri huongoza waumini kuanza kukumbuka maelezo ya siku ambayo Yesu Kristo alitoa Sakramenti katika Chakula cha Mwisho kwa wanafunzi wake akitaka wamkumbuke.
Kwa kawaida, eneo hilo ndipo Padri kwa mamlaka aliyopewa, hufanya mageuzi ya sakramenti kuwa Hostia Takatifu, kwa maneno mengine hubariki mkate kuwa Mwili wa Kristo na divai kuwa Damu ya Kristo.
Kwa Wakatoliki, eneo la mageuzi ni eneo muhimu na ndio waumini hutuma maombi kimya kimya, wakiamini ndio Kristo anashuka mwenyewe.
Baada ya kutumikia Kanisa na kukubalika, Asenga aliaga kuwa anarudi nchini Marekani kwa kuwa muda wake wa mapumziko, umekwisha na kuagwa na Kanisa.
Taarifa tata Wakati uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria Madeko, ukiwa na imani kuwa Asenga ni Padri na amerejea New York, kuendelea na Utume, walipata taarifa za kushangaza kutoka kwa baadhi ya waumini, wakidai wamekutana na Asenga mitaani.
Mbali na taarifa hiyo ya kukutwa mitaani na waumini wake, taarifa zaidi zilieleza kuwa amekuwa akiishi na mwanamke katika eneo la Ujenzi, kinyume na desturi za mapadri wa Kanisa Katoliki duniani, ambao hawaruhusiwi kuoa.
*Mtego 1
Baada ya taarifa hizo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, Asenga aliwekewa mtego na Paroko wa Parokia hiyo ya Mtakatifu Maria Madeko, Malt Dyfrig Joseph.
Paroko huyo inadaiwa aliwaomba waumini wamshawishi Asenga afike parokiani hapo na baada ya kufika, alihojiwa na Paroko huyo na kudai kuwa alipata upadirisho katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya Paroko huyo kupata maelezo hayo, alifanya mawasiliano na Katibu wa Jimbo hilo la Dar es Salaam na kujibiwa kuwa hakuna jina la Padri huyo.
Kukamatwa, akiri Mtego wa pili kwa mujibu wa Kamanda Paulo, ulifuata kwa Paroko huyo kutoa taarifa Polisi kuhusu uwepo wa Padri feki, ambaye aliaminiwa kwa kiwango cha kuruhusiwa kuongoza Misa.
Taarifa hizo zinasema Alhamisi ya wiki hii, saa 10:30 jioni, Asenga alimpigia simu Paroko huyo na kuomba ampangie kazi ya kuendesha Misa Jumapili ya leo parokiani hapo, na kukubaliwa ambapo Paroko huyo alimtaka afike kanisani.
Baada ya kufika, taratibu za kujulisha Polisi zilifanywa na askari walipofika kanisani hapo, walimkamata mtuhumiwa huyo. Kwa mujibu wa Kamanda Paulo, baada ya kufanya mahojiano na Asenga, alikiri kuwa yeye si Padri na walipokwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi, walimkuta akiwa na majoho saba ya upadri.
Mikoani, mafunzo Taarifa zaidi zilizofikia gazeti hili jana, zilibainisha kuwa Asenga huenda kwa kutumia mbinu hizo hizo, alishaaminiwa kuongoza Misa katika mkoa wa Kilimanjaro katika maeneo ya Uru na Moshi na mkoani Singida.
Mbali na kukubalika katika mikoa hiyo, lakini taarifa zaidi zilibainisha kuwa Asenga alifanikiwa kote huko kuongoza Misa na kuaminiwa, kutokana na mafunzo ambayo aliwahi kupata huko nyuma.
Inadaiwa Asenga alianza kupata mafunzo katika Seminari ya Kanisa Katoliki ya Uru, ambako alipata mafunzo ya elimu ya sekondari.
Baada ya kumaliza kwa mafanikio masomo yake katika seminari hiyo, alichaguliwa kujiunga na Seminari ya Kibosho, ambayo inatajwa kuwa maalumu kwa ajili ya kutoa elimu ya falsafa kwa wanafunzi na wengi ni wanaotarajiwa kuwa mapadri.
Mafanikio aliyoyapata katika masomo ya falsafa katika Seminari ya Kibosho, yalimwezesha kujiunga na Seminari ya Kipalapala, ambako inaelezwa ndiko kunakotolewa mafunzo ya Liturgia, ambayo nayo ni sehemu ya mafunzo wapewayo wanafunzi wanaotarajiwa kuwa mapadri.
Waumini Ingawa taarifa za mafunzo aliyopata zinatiliwa shaka, lakini namna alivyoongoza Misa bila kutiliwa shaka, imesababisha baadhi ya waumini kuanza kumjadili, ili kufahamu hasa nia yake ilikuwa ipi.
Kutokana na taaluma nyingine aliyonayo ya uhasibu, amesababisha baadhi ya waumini kuunganisha matukio na uwezo wake na kuamini kuwa huenda hakuwa akitafuta sadaka.
Mmoja wa waumini aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, alidai kuwa huenda Asenga alikuwa na njama za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Kwa mujibu wa madai ya muumini huyo, watu wa aina ya Asenga, ambaye ana taaluma na uwezo wa kipadri, wana njia nyingi za kujipatia kipato, hivyo inawezekana alidanganya wafadhili wake kuwa yeye ni Padri ili apate ufadhili huo.
Muumini huyo alikwenda mbali na kudai huenda masharti ya ufadhili huo, ni kupata picha au sauti yake akiongoza Misa kanisani.
“Inawezekana kuna mahali aliomba ufadhili kwa ajili ya kitu fulani na aliwadanganya kuwa yeye ni Padri, ndio maana akaamua kuomba zamu ya kuongoza Misa.
“Utapeli umeingia mpaka kwenye nyumba za ibada kweli? Wanadamu tumekosa hofu ya Mungu!” Alihoji muumini huyo na kuasa jamii kuwa macho, kwa kuwa hivi sasa matapeli ni wengi na kila siku wanatoka na mbinu mpya.
Credit:Habari Leo
No comments:
Post a Comment