Tuesday, June 26, 2012
Mbunge ataja majina ya 'wezi' bungeni
MBUNGE wa Viti Maalum, Riziki Lulida (CCM) leo ametaja bungeni majina ya watendaji wa Halmashauri nchini wanaodaiwa kuiba mamilioni ya fedha za Serikali. Mbunge huyo amepinga kitendo cha mmoja wa watendaji hao kuhamishiwa mkoani Lindi na amesema, mkoa huo si kichaka cha wezi. Ametaja jina la Joachim Materu, na kudai kuwa, mtumishi huyo wa umma aliiba shilingi milioni 557 za umma na amehamishiwa mkoani Lindi. Amewaeleza wabunge kuwa, kitendo cha kuwahamisha wanaodaiwa kuwa ni wezi kutoka Halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine ni njama za kudhoofisha maendeleo ya maeneo wanapopelekwa. Lulida amekataa kuunga mkono bejeti ya Waziri Mkuu hadi Materu ahamishwe Lindi. Mbunge huyo amesema kuwa, kuna maofisa mipango Ofisi ya Waziri Mkuu wanaouhujumu Mkoa
wa Lindi. Lulida amedai kuwa maofisa hao ni wachaga, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), akaomba Kiti cha Spika kimuamuru afute kauli yake ya kutaja kabila la wahusika kwa kuwa Kanuni za Bunge haziruhusu, amefuta. “Suala la uchaga halimo lakini nimetaja majina ili uonekane mtandao”amesema Mbunge huyo wakati anachangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mbunge huyo amemtaja mtendaji mwingine kwa jina la Yunus Maro, na kudai kuwa, ameiba shilingi milioni 262 za umma, na kutaja akaunti yake ni namba 20660017 iliyopo katika benki ya NMB. Ametaja jina lingine moja la Ndaskoi na kudai kuwa
mtumishi huyo ameiba fedha za umma wilayani kilosa mkoani Morogoro na amehamishiwa Ngorongoro. Amemtaja mwingine kwa jina la Macha na kudai kuwa, ameiba mamilioni wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, na ametoa vielelezo kwenye kiti cha Spika wa Bunge kuthibitisha anayoyasema. Lulida amedai kuwa kuna mtandao wa wezi katika Halmashauri nchi wanaoihujumu Serikali. Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM) ameunga mkono kauli ya Lulida kwamba kuna mtandao wa wezi katika Halmashauri nchini. “Huu mtandao ndiyo unaodhoofisha Mkoa wa Lindi” amesema Mtanda wakati anachangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Hata hivyo Mtanda amepinga suala la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuonesha kinawajali sana wananchi wa mikoa ya kusini ukiwemo Mkoa wa Lindi. Amesema, ameisoma Ilani ya Uchaguzi ya Chadema, imeutaja mkoa huo mara moja tu, lakini katika Ilani ya CCM mkoa huo umetajwa mara nane. “Hatutaki ndoa za usiku, asubuhi talaka” amesema Mtanda na kuhoji, Chadema walikuwa wapi miaka iliyopita? “Mheshimiwa unapolia hushiki kichwa cha mwenzio, sisi Lindi matatizo yetu tutayamaliza sisi kwa kushirikiana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi” amesema Mtanda.
....
Source Habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment