Monday, July 25, 2011

Chadema yahaha kutatua mgogoro wa madiwani Arusha

KATIKA kile kinachoonekana ni
kutafuta suluhu ya mgogoro wa
madiwani wa Chadema katika
Halmashauri ya Jiji la Arusha,
Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe amefika hapa
juzi kwa lengo la kukutana nao.
Hata hivyo, hakufanikiwa kwani
alishauriwa kutozungumzia
mgogoro huo kwa kuwa yupo
katika ngazi ya Kamati Kuu ya
chama hicho.
"Ni kweli Mbowe alikuwapo hapa
tangu Jumamosi, lengo lake
lilikuwa kukutana na madiwani
hao lakini baadaye alishauriwa
kuwa asifanye hivyo kwa kuwa
yeye ni Mwenyekiti wa Kamati
Kuu ya Chama," mmoja wa
wabunge wa Chadema Kanda ya
Kaskazini, alilieleza gazeti hili kwa
sharti la kutotajwa jina gazetini
na kuongeza:,
“Mwenyekiti yuko hapa, nadhani
atakutana na madiwani
wanaovutana na viongozi wa
kitaifa akiwamo Katibu Mkuu, Dk
Willibrod Slaa kuhusu hatua yao
ya kufikia muafaka na kukubali
baadhi ya nyadhifa ndani ya
Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Manispaa ya
Arusha,” alisema mtoa habari
wetu kwa sharti la kutotajwa
gazetini.
Pamoja na mambo mengine,
mwenyekiti huyo ambaye pia ni
kiongozi wa kambi rasmi ya
upinzani bungeni alitarajiwa
kusikiliza hoja za madiwani hao
na kujadiliana nao kutafuta njia
nzuri na sahihi za kuchukua
badala ya kutunishiana misuli na
vikao vya uamuzi, kama
ilivyojitokeza kwa walioamriwa
kujiuzulu nyadhifa zilizopatikana
kutokana na muafaka wa umeya
wa jiji hilo.
Kikao cha CC ya Chadema kiliagiza
madiwani waliopata nyadhifa za
unaibu meya na uenyekiti wa
kamati kujiuzulu nafasi hizo
ndani ya siku tatu kufikia Julai
21, mwaka huu. Madiwani hao
wakiongozwa na Estomih Mallah
wa Kata ya Kimandolu na John
Bayo wa Kata ya Elerai
wamegoma kutekeleza agizo hilo
na badala yake nao wakatoa
masharti ya kuombwa radhi na
Dk Slaa na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema kwa madai
ya kudhadhalilishwa kwa
tuhuma za kula rushwa ili kufikia
muafaka huo na CCM.
Kwa mujibu wa mbunge huyo,
wakati jitihada za Mbowe
zikigonga mwamba, mwasisi wa
Chadema, Edwin Mtei amechukua
hatua za makusudi kumaliza
mgogoro huo kwa kuzungumza
kwa nyakati tofauti na pande
zote zinazovutana. Mtei
amekutana na madiwani hao,
Lema na uongozi wa Chadema
kuzungumzia mgogoro huo
akitaka pande hizo zinazovutana
zimalize tofuati zao kwa busara.
Mtei alikutana na madiwani hao
baada ya kumwomba afanye
hivyo ili kuumaliza kwa amani
badala ya kuvutana hadharani.
Madiwani hao wa Chadema
wilayani Arusha walikutana na
Mtei nyumbani kwake Tengeru
nje kidogo ya jiji la Arusha
mwishoni mwa wiki na kuomba
ushauri juu ya mvutano huo
unaoendelea kukipasua chama
hicho.
Alipotakiwa kuzungumzia suala
hilo, Mtei hakukiri wala kukataa
kukutana na madiwani hao.
Alisisitiza kuwa Chadema
hakiwezi kumeguka kutokana na
mgogoro huo. "Sisi (Chadema)
tuna mipango na sera zenye
matumaini kwa Watanzania,
hatuwezi kumeguka kwa
mgogoro huo."
Hata hivyo, Mtei aliwataka
viongozi wa Chadema, madiwani
wake na Lema kutumia busara
na kupunguza jazba katika
kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
.
.
.
>>Habari kutoka katika Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment