BUNGE la Tanzania linakoelekea
sasa si kuzuri. Pengine ndivyo
inavyoweza kuzungumzwa
kuhusu mambo yanavyokwenda
ndani ya chombo hicho cha
kutunga sheria na kuisimamia
Serikali.
Hali hiyo inatokana na tukio la
juzi usiku baada ya wabunge au
Mbunge asiyefahamika, kughushi
saini ya Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, wakati kikao kikiendelea.
Aliyeweka wazi aibu hiyo ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,
William Lukuvi, muda mfupi
baada ya Bunge kupitisha
Makadirio ya Matumizi ya Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kwa Mwaka 2011/12
yaliyowasilishwa Jumatatu na
Waziri Profesa Jumanne
Maghembe, ambapo Sh. bilioni
258.3 ziliidhinishwa.
Baada ya Mwenyekiti wa Bunge,
ambaye pia ni Mbunge wa
Kibakwe, George Simbachawene
(CCM) kuzungumzia kupitishwa
kwa bajeti hiyo na kumpongeza
Waziri na wabunge, huku
akijiandaa kusitisha shughuli za
Bunge ikiwa ni karibu saa 2:15
usiku, alisimama Waziri Lukuvi na
kuomba Mwongozo wa
Mwenyekiti.
Katika maelezo yake ya kuomba
Mwongozo, Lukuvi alisema
kumeibuka tabia ndani ya Bunge
ambayo si ya kistarabu, kwani
baadhi ya wabunge wamekuwa
wakiandika ujumbe kwenye
vikaratasi kuonesha mhusika
fulani anaitwa wakati hakuna
jambo kama hilo.
“Kwa leo (juzi) hapa yametokea
matukio mawili ya wabunge
Joseph Selasini (Rombo-
Chadema) na Leticia Nyerere (Viti
Maalumu-Chadema) kupelekewa
ujumbe kwa nyakati tofauti
ukionesha umesainiwa na Waziri
Mkuu akiwaita.
“Lakini jambo la ajabu Waziri
Mkuu mwenyewe hajui lolote na
anashangaa jambo hili maana
hakuandika ujumbe kuwaita,”
alisema Waziri Lukuvi na
kusababisha mshangao kwa
baadhi ya wabunge.
Kutokana na mazingira hayo,
aliomba suala hilo liachwe na
kwamba si tabia nzuri ambayo
imeanza kujitokeza.
Akizungumzia suala hilo,
Simbachawene naye alilaani
jambo hilo na kusema kwa vile
karatasi iliyoandikwa alikuwa
nayo, itakuwa rahisi kumbaini
mhusika na kumshughulikia.
“Karatasi yenyewe imeandikwa
hivi: Mheshimiwa Joseph Selasini,
naomba uje kuna jambo tujadili,
nahitaji ufafanuzi kutoka kwako
- Mizengo Pinda,” alisema
Simbachawene na kuongeza
kuwa karatasi hiyo imesainiwa
kuonesha aliyesaini ni Waziri
Mkuu.
“Ndiyo maana nilimwona
Mheshimiwa Selasini amekwenda
kwa Waziri Mkuu akiwa
amejikunyata kistaarabu kuona
ameitiwa kitu gani, lakini
Mheshimiwa Waziri Mkuu wala
alikuwa hamfuatilii, alikuwa
ameelekeza mawazo yake katika
majibu ya Waziri,” alisema
Mwenyekiti huyo.
Alieleza kuwa jambo hilo ni la
aibu kubwa kwa wabunge,
kufikia hatua ya kughushi saini
ya Waziri Mkuu na kusisitiza
lazima ichukuliwe uzito
unaostahili.
Tangu Bunge la 10 lianze,
kumekuwa na malalamiko
kutoka kwa wadau mbalimbali
kwamba limepoteza heshima
kutokana na baadhi ya wabunge
kufanya mambo ambayo
hayaendani na chombo hicho –
ya kitoto.
Masuala ya kuzomeana, kupigana
vijembe na wakati mwingine
kuzungumza bila mpangilio, ni
baadhi ya mambo yanayopigiwa
kelele na wadau kwamba
yanakivunjia heshima chombo
hicho, ambacho ni moja ya
mihimili mikuu mitatu ya Dola.
No comments:
Post a Comment