Sunday, August 12, 2012
ULIMBOKA AREJEA NCHINI AKIWA FITI
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari, Dk
Steven Ulimboka amerejea nchini jana
akitokea Afrika Kusini alikopelekwa kwa
matibabu na kusema amepona kabisa.
Ulimboka, ambaye alikuwa anaratibu
migomo ya madaktari iliyofanyika mara
mbili mfululizo, alitekwa na watu
wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatano
ya Juni 27, mwaka huu na kupelekwa katika
msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam, ambako aliteswa na kujeruhiwa
vibaya.
Katika tukio hilo, daktari huyo aling’olewa
meno mawili na kucha za mkono mmoja na
baadaye kulazwa katika Kitengo cha
Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu
(ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI) katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya, Juni
30, mwaka huu, alisafirishwa kwenda Afrika
Kusini kwa ajili ya vipimo na matibabu.
Dk Ulimboka aliwasili jana saa nane mchana
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), akitembea mwenyewe
na kulakiwa na mamia ya wananchi wa Jiji
la Dar es Salaam, wakiwamo madaktari
wenzake pamoja na wanaharakati.
Huku akibubujikwa na machozi pamoja na
ndugu zake, madaktari na wanaharakati
nao walimpokea kwa machozi kisha
walimkinga kiasi ambacho kulitokea vurugu
za kila mmoja kutaka kumwona.
Akizungumza kwa ujasiri huku akizongwa
na madaktari pamoja na wanahabari,
Ulimbona alianza kwa kuwashukuru wote
waliofika kumpokea na pia kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kufikisha katika hali
aliyonayo sasa pamoja na Chama cha
Madaktari waliosaidia kupata fedha za
matibabu.
Alisema kwa sasa afya yake imeimarika na
amepona kabisa na yuko tayari kufanya
jambo lolote bila utata na kuruhusu maswali
kwa wanahabari, lakini madaktari wenzake
walikataa na kumtaka aende kwenye gari ili
aondoke kwenda kupumzika. Alitii agizo hilo
na kuondoka kwenda kwenye gari.
Awali, kabla Dk Ulimboka hajawasili JNIA, nje
ya uwanja wa ndege madaktari pamoja na
wanaharakati walisikika wakiimba nyimbo
mbalimbali zikiwamo za ‘Tanzania
Nakupenda, ‘Kama siyo juhudi zako Nyerere’
pamoja na kuhamasishana kuwa Solidarity
Forever (Mshikamano Daima).
Baada ya kutembea hatua chache na kufika
lilipokuwa gari lililombeba, Dk Ulimboka
alisimama na kutaka kuzungumza jambo na
wanahabari, lakini madaktari na nduguze
walimkataza tena na kudai wamuache ili
aende kupumzika.
Katibu wa Jumuiya hiyo ya Madaktari, Dk
Edwin Chitage akizungumzia gharama za
matibabu ya Dk Ulimboka, alisema
wanazikusanya na kujumlisha na
watazieleza hivi karibuni kwa vyombo vya
habari.
Wanaharakati waliokuwapo uwanjani hapo,
walizungumzia kurejea kwa Dk Ulimboka na
kudai mapambano yameanza upya, kwani
kilichomfanya daktari huyo kupigwa ni
kupigania maslahi ya Watanzania wote.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari
Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya alisema
umefika wakati wa Watanzania kusimama
na kuacha woga na unafiki katika kupigania
haki za afya zao.
Nkya alisisitiza kuwa mapambano
aliyoyaanzisha Dk Ulimboka yanaendelea.
Jambo lililoungwa mkono na Mkurugenzi
Mtendaji wa TGNP, Usu Malya alisema
mapambano ya Dk Ulimboka ni ya
Watanzania wote, hivyo kila mmoja
anatakiwa kumuunga mkono.
Dk Ulimboka alitekwa na kuumizwa vibaya
wakati mgomo wa madaktari nchini ukiwa
unaendelea, na tangu wakati huo baadhi ya
wanasiasa hasa wa upinzani, na
wanaharakati wamekuwa wakiituhumu
Serikali kuhusika katika kutekwa na
kupigwa kwa daktari huyo.
Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Rais Jakaya
Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
mara kadhaa baada ya tukio hilo, imesisitiza
kuwa haihusiki na unyama huo, na wala
haikuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Tayari raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21)
amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akituhumiwa
kumteka na kufanya jaribio la kumwua Dk
Ulimboka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment