Friday, July 1, 2011

PINDA AMJIBU LOWASA

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda
ameliambia Bunge kuwa serikali
ya Awamu ya Nne haiogopi
kufanya maamuzi na
imeshafanya maamuzi mengi
magumu.
Alikuwa akijibu hoja za wabunge
waliochangia hotuba ya bajeti ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu,
Edward Lowassa ambaye
aliituhumu Serikali kwa
kushindwa kufanya maamuzi
magumu.
Akizungumza kwa mara ya
kwanza bungeni tangu
alipojiuzulu wadhifa huo kwa
kashfa ya Richmond Februari 7
mwaka 2008, Lowassa
aliishangaa Serikali kwa kuogopa
kufanya maamuzi.
Lowassa aliyeshika Uwaziri Mkuu
Desemba 30, mwaka 2005 akiwa
Waziri Mkuu wa Kumi nchini,
akiichambua zaidi Serikali
bungeni hivi karibuni alisema
viongozi wa Serikali wameingiwa
na ugonjwa wa kuogopa kutoa
maamuzi kwa mambo
mbalimbali hatua inayokwamisha
utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Lakini katika majibu yake ya jana
jioni, Pinda alisema Serikali haina
cha kuogopa na kwamba tayari
imeshafanya maamuzi mengi
tena mengine ni magumu.
Alisema moja ya maamuzi hayo
ni uamuzi wa kuvunja Baraza la
Mawaziri uliotokana na yeye
Lowassa kujiuzulu.
“Halikuwa jambo jepesi hata
kidogo bali ni moja ya maamuzi
mazito ambayo yamefanywa na
Serikali ya Awamu ya Nne.
Inataka Moyo…” alisema Pinda.
Pinda alisema maamuzi hayo ni
sehemu ya maisha ya Serikali
katika kutekeleza majukumu
yake kwa dhana ya Uwajibikaji
wa pamoja, yaani Collective
Responsibility kupitia Baraza la
Mawaziri.
“Tunachohitaji ni kuvumiliana.
Kuvuta subira, kwani mambo
mema hayataki haraka!
Tutaamua na tutafanya,” alisema
Pinda na kuongeza; “Napenda
kulifahamisha Bunge lako Tukufu
kwamba Serikali ya Awamu ya
Nne chini ya Mheshimiwa Rais
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ndiyo
pekee imefanya maamuzi
magumu na mazito kuliko zote
zilizopita.”
Aliyataja maamuzi mengine kuwa
ni pamoja kuimarisha Utawala
Bora, akitolea mfano uamuzi
mgumu wa kuwafikisha
mahakamani waliokuwa
mawaziri wa Serikali zilizopita
kutokana na tuhuma mbalimbali
zinazowakabili za kutumia
madaraka isivyo halali.
Baadhi ya mawaziri wa Awamu
ya Tatu waliofikishwa
mahakamani kutokana za
matumizi mabaya ya madaraka ni
pamoja na Basil Mramba
aliyekuwa Waziri wa Fedha na
Daniel Yona (Nishati na Madini)
na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Pinda aliendelea kusema
kwamba, Serikali ya Awamu ya
Nne ndiyo iliyoamua kujenga
shule za sekondari za Kata
ambazo zimewezesha wanafunzi
wengi kupata elimu ya
sekondari.
“Leo tumeshuhudia kuwa kati ya
wanafunzi 20 tuliowapongeza
kwa kufanya vizuri kwenye
mitihani ya kidato cha sita 2011,
saba (7) wanatoka shule za Kata,
sawa na asilimia 35,” alisema.
Aliongeza kuwa, wameweka
historia ya kuamua kujenga Chuo
Kikuu cha Dodoma ambacho ni
kikubwa mno nchini na kwamba
faida yake inaonekana, kwani
tayari zaidi ya wanafunzi 20,000
wanasoma kwa sasa.
“Ninaamini kila mmoja kati yetu
humu ndani anaye mtoto, awe
mjukuu, mjomba, shangazi, baba
mdogo, ndugu, jamaa na hata
rafiki tu ambaye anasoma katika
chuo hiki.
Ndiyo sababu kubwa
inayotufanya wote tuone
uchungu wa baadhi ya watu
wanaowasumbua hivyo
kusababisha watoto wetu
washindwe kukamilisha masomo
yao kwa wakati kutokana na
migomo inayojitokeza mara kwa
mara.
“Aidha, tunajenga Chuo cha
Serikali za Mitaa Hombolo
ambacho kimefikia hatua nzuri,”
alisema Pinda na kuongeza kuwa
Serikali ya Awamu ya Nne
imekamilisha miradi yote 27 ya
barabara kuu zilizoanzishwa na
Serikali ya Awamu ya Tatu.
Sasa hivi unaweza kutoka
Mtwara-Dar es Salaam-Dodoma
hadi Mwanza kwa kupitia
kwenye barabara ya lami.
Alisema pia kwamba, Serikali
imeamua fedha zote za MCC
zipelekwe kujenga barabara za
mikoa iliyoko pembezoni.
“Tumeshuhudia ndani ya Bunge
hili waheshimiwa wabunge, bila
ya kujali itikadi za vyama
wakisifu maendeleo
yaliyopatikana kule Kigoma.
Maamuzi mengine ni Ujenzi na
ukamilishaji wa miradi ya maji
cchini. Tumefanya maamuzi
mazito katika kuwalinda watu
wenye ulemavu wa ngozi na
tumefanikiwa,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ili kuondoa
mpasuko wa kisiasa Zanzibar,
“tumefanya maamuzi magumu
ya kukubali kuanzisha Serikali ya
Umoja wa Kitaifa katika Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar.


KWA HABARI KAMILI SOMA GAZETI LA HABARI LEO LA KESHO

No comments:

Post a Comment