Thursday, June 30, 2011

MADIWANI JINO KWA JINO NA DK SLAA

MADIWANI wa Chadema katika
Manispaa ya Arusha, wamesema
chama hicho ‘hakina ubavu’ wa
kuwafukuza kwa kuwa kufanya
hivyo, kitakuwa kinacheza
mchezo wa pata potea.
Wakizungumza na Gazeti la Habari leo la nchini Tanzania kwa
masharti ya kutotajwa majina
gazetini baada ya kuonywa
kutozungumzia mgogoro wao
na uongozi wa chama hicho
Taifa, madiwani hao walisema
wanaamini Kamati Kuu ya chama
hicho haiwezi kufanya kosa hilo.
‘’Hili suala linapaswa kuamuliwa
kwa hekima na busara,
kunifukuza mimi ama madiwani
wote hapa kuna mambo mawili;
moja Chadema kupoteza viti
vyote ama kupata na hiyo ni
bahati nasibu na sidhani kama
Kamati Kuu italikubali hilo,’’
alisema mmoja wa madiwani
hao.
Juni 29 Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Willibrod Slaa,
alikaririwa akisema chama hicho
kiko tayari kuwatimua madiwani
wake wote wa Arusha kwa
madai kuwa wamekisaliti chama
baada ya kufikia muafaka wa
Arusha kwa maslahi ya mkoa
huo.
Dk. Slaa alikaririwa, akisema
uamuzi wa madiwani huo,
kumpata meya na naibu wake
Arusha ambao ulipongezwa na
Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), hawautambui kwa
madai una upungufu ukiwamo
wa kukosa barua ya Chadema ya
kukubali maridhiano.
Baada ya kauli hiyo ya Dk. Slaa,
iliyotolewa baada ya kauli
nyingine ya Mbunge wa Arusha,
Godbless Lema, kwamba
hatambui maridhiano hayo ya
amani na yenye lengo la
kuharakisha maendeleo ya
Arusha, madiwani hao Juni 30
waliweka kikao katika hoteli
moja
kubwa mjini hapa kujadili kauli
hizo.
Baada ya kikao hicho, diwani
mwingine alisema Dk. Slaa
amewatumia ujumbe kwa njia ya
mtandao wa intaneti na
kuwaamuru waache
kuzungumzia suala hilo katika
vyombo vya habari.
Alisema hata hivyo, kikao chao
kimesisitiza kuwa muafaka
waliofikia na madiwani wenzao
wa CCM, ni sahihi uliofuata
taratibu zote kwa maslahi ya
chama na si uamuzi wa mtu
binafsi wenye uroho wa
madaraka na kamwe
hawakukurupuka.
‘’Tumefikia muafaka kwa maslahi
ya Chadema pia, hatukufanya
hivyo kwa uroho wa kutaka vyeo
katika kamati ndani ya
Halmashauri.
Kauli kwamba tuliamua kwa
uroho wa madaraka ni kutaka
kuupotosha umma na kauli hizo
hazifai kutamkwa na kiongozi
kama Lema,’’ alisema diwani
huyo.
Alisema wanawaheshimu sana
viongozi wao wa juu, lakini na
wao ni viongozi waliochaguliwa
na wananchi kama Lema na
uamuzi waliochukua Lema
anaujua, lakini inasikitisha kuona
madiwani wakiamua ni kosa,
wakati ni kwa maslahi ya wakazi
wa Arusha.
Diwani huyo alidai Lema anajua
kila kitu, kwa kuwa katika
mchakato wa awali,
alishirikishwa na kuambiwa kila
kitu kinachoendelea, lakini
hakutoa uamuzi ila
kinachoonekana ni ubinafsi
wake na huo ndio unaosumbua
ndani ya Chadema.
‘’Hapa suala ni kutoa uamuzi kwa
maslahi ya chama na si mtu
binafsi; hilo halitawezekana,
kwani kila mmoja anapaswa
kuheshimiwa na kusikilizwa
katika kutoa uamuzi na
wasitokee baadhi ya watu ndani
ya chama kuonekana miungu
watu,’’ alisema.
Mbali na Dk. Slaa na Lema, pia
Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe, alinukuliwa
kwa nyakati tofauti akipinga
muafaka huo.
KWA HABARI ZA UHAKIKA ZAIDI SOMA GAZETI LA HABARI LEO!

No comments:

Post a Comment