Tuesday, June 26, 2012

Mbunge ataka vigogo wauziwemashangingi

MBUNGE wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM) amesema, magari ya Serikali yanatumiwa vibaya hivyo yauzwe kwa watumishi wa umma ili kupunguza matumizi yasiyo na tija. Mbunge huyo amesema, Serikali itumie waraka uliotolewa wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili kuyauza magari hayo kwa watumishi, na kwamba, kila anayestahili apewe gari kulingana na kazi anazofanya na wadhifa wake. “Nilikuwa najiuliza, waraka ule ulifutwa au umepitwa na wakati? “ ameuliza Mbunge huyo bungeni mjini Dodoma wakati anachangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa Mbunge huyo, licha ya Serikali kutoa waraka huo, magari ya Serikali yalitumika kufanya kazi binafsi za watumishi wa umma, na zikaandaliwa bajeti za kununua magari mengine ya Serikali. Mlata amesema, itakuwa busara kama Serikali itayauza magari hayo kupunguza matumizi ya Serikali na amedai kuwa Tanzania ni nchi pekee Afrika Mashariki inayotumia magari isivyostahili. Mbunge huyo ameliembia Bunge kuwa, huwa anasikia aibu wakati wa sherehe za kitaifa, kwa kuwa mabalozi wa nchi wahisani huwa wanakwenda uwanjani wakiwa kwenye gari la pamoja lakini viongozi Watanzania huwa wanashindana kwa magari. Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema) amesema, uamuzi wa Serikali, kuweka ukomo wa ukubwa wa injini za magari yanayoweza kununuliwa na Serikali Kuu, taasisi zake na mamlaka za Serikali za Mitaa hautakuwa na tija kama magari ya kifahari yaliyopo sasa hayatauzwa. “Haya yangeuzwa halafu tukanunua mengine” amesema Nyerere bungeni mjini Dodoma wakati anachangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza bungeni uamuzi wa Serikali kuweka ukomo huo ili kupunguza matumizi yasiyo na tija. Pinda, amelieleza Bunge kuwa, Serikali inaendelea kupunguza matumizi hayo hasa ununuzi wa magari makubwa na ya kifahari ambayo gharama za ununuzi na uendeshaji ni kubwa sana. Waziri Mkuu amewaeleza wabunge kuwa, kuanzia sasa magari yatakayonunuliwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa CC 3,000 kwa viongozi na watendaji wakuu na yasiyozidi CC 2,000 kwa watumishi wengine wanaostahili kutumia magari ya serikali. Kwa mujibu wa Pinda, ili kupunguza matumizi ya magari kwa viongozi na watendaji wakuu kwa safari za mikoani, Serikali itaanzisha vituo vya kanda vya magari ya serikali yatakayotumika mikoani kwa shughuli za kikazi. “Mwongozo wa utekelezaji utatolewa. Inategemewa kuwa utaratibu huu utapunguza matumizi ya fedha za Serikali kwa kiwango kikubwa” amesema Pinda bungeni mjini Dodoma wakati anasoma mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema), amesema, kuna watanzania wanaishi kama wafalme na kuna matumizi yasiyo ya kawaida serikalini. Wenje amehoji, wakuu wa mikoa yote nchini wamekwenda Dodoma kufanya nini? Zimetumika fedha nyingi kuwasafirisha, wanalipwa fedha za safari na wanakaa bungeni ‘kula kiyoyozi’ bila sababu za msingi. Kwa mujibu wa Wenje, wakuu wa mikoa wapo Dodoma tangu Jumamosi iliyopita, na wameacha kazi walipotoka. “Wakuu wa mikoa wamekuja kufanya nini? Wamekuja kutafuta nini, wamekuja kutafuta nini?” amehoji Wenje na kusema, Serikali inapaswa kubadili mbinu za kiutendaji.

No comments:

Post a Comment