Thursday, June 28, 2012

Ni ipi siri ya Muungano,Watanganyikawanaogopa nini ?

Leo ni takriban miaka 48 ya Muungano kati ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Tanganyika tokea kuasisiwa kwake baada ya Mapinduzi,lakini kwa walio wengi hususani Wazanzibar wameshindwa hasa kujua ni ipi hasa siri ya Muungano huu.Kumekuwa na madai mengi na fikra tofauti kuhusu Muungano huu kutoka kwa watu na taasisi mbali mbali ndani na nje ya nchi. Ni dhahiri kwamba mwisho wa yote Muungano huu utamalizika au utaendelea mbele ukiwa na uhasama mkubwa kuliko udugu,upendo,maelewano na maendeleo kama wanavyodai wale wote wenye hoja ambazo wanautetea Muungano huu wenye hila na siri nzito, hususani Viongozi wa Serikali walioko madarakani wale wa Bara na baadhi ya wale Wahafidhina wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,ambao hutumiwa kama chambo zidi ya Wazanzibar wenzao. Katika Muungano huu tokea siku ya mwanzo , kumekuwa na tuhuma nyingi kiasi ambacho kwa mwenye akili timamu hatosita kuelewa kwamba ndani yake kuna siri nzito zidi ya Taifa moja. Kwa walio wengi wanakumbuka kwamba unapolitaja neno Muungano hapo zamani ilikuwa ni kosa la jinai na adhabu yake kwa wakati huo ilikuwa kifo.Wako Wazanzibar wengi ambao walikuwa Wasomi,wanafalsafa,wanasiasa,madokta pamoja na Wananchi wa kawaida walipoteza maisha yao kwa kupinga au kuhoji Muungano huu,lakini kama haya hayatoshi hadi hii leo bado Wazanzibar wanaonekana kama ni maadui pale tu wanapoligusia suala zima la kudai haki yao ndani ya Muungano. Tuangalie kama vile jumuia ya Uamsho ambayo imejitolea kwa ridhaa yao kuwaelimisha Wananchi juu ya haki zao za msingi kudai Nchi yao huku wakifuata sheria za Nchi,hapa pana kuna kosa gani kwa Mwananchi kujielewa na kujua haki zake za msingi? Nilifikiria ya kwamba Serikali zote mbili zitawapongeza kwa vile Jumuiya hiyo imejitolea kihali na mali kutoa elimu kwa Wazanzibar, jambo ambalo Serikali zote mbili zimeshindwa kulifanya kwa Wananchi wake. Kichekesho ni kuona Muungano huu wa Nchi mbili huru, mara zote wanaolalamika kuonewa ni upande mmoja wa Muunganoyaani Zanzibar, lakini zaidi wanaopiga kelele kwa kuumia ni wananchi wanyonge walio wengi na si Viongozi wa Serikali zote mbili.Pia la ajabu ni kwamba Watanganyika wamerizika na wala Wananchi wake hawana madai kwamba wanaonewa na zaidi wanapendelea Muungano huu uzidi kuimarika. Hapa tutapata picha halisi kwamba ni dhahiri Watanganyika wanafaidika sana na hali hii iliopo hivi sasa.Isitoshe Watanganyika mara zote hutoa vitisho kwamba pindipo Muungano ukivunjika basi Zanzibar na hasa Wapemba ndio watakaoumia kwa vile wamejiimarisha sana huko wamejenga magorofa, hii inaonesha kwamba kuna lengo la kuwafukuza Wazanzibar Tanganyika kama kuwapa adhabu, watu wanasahau historia kwani Zanzibar baada ya Mapinduzi baadhi ya watu walinyang’anywa majumba yao, mashamba na vyenginevyo na hadi sasa watu wanaishi. Sasa huo udugu unaozungumziwa na Watanganyika ndio huo ? Jee wale Wazanzibar au Watanganyika wanaoishi United kingdom,Canada,Marekani,Falme za kiarabu nao pia warejeshwe maanake hawa wote hawakuungana na Nchi hizo, nako huko pia wamejiimarisha hizo ni propaganda za kijinga na ulimbukeni. Nashindwa kuelewa kuona Watu ambao wanajiita Wasomi wa Watanzania wakiwemo , Marais,Mawaziri,Wabunge,Wawakilishi na Waandishi wa habari wanashindwa kufahamu maana ya Nchi kuwa huru,haki za binaadamu,uhuru wa kuabudu,demokrasia ya kweli,usawa kwa wote, lakini pia dhana ya Muuungano kwa Nchi husika ni nini. Naamini wangalifahamu dhana hizi basi wangeliondokana na zile kasumba na fikra za ukandamizaji zilizoletwa na Wakoloni weupe na baadae kurithishwa kwa Wakoloni weusi kama vile Mwalimu Nyerere na baadhi ya Viongozi wa Afrika ambao kwao wao mabadiliko ya kidemokrasia ni mwiko. Sisi kama kizazi kipya tunaenda kwa misingi ya mabadiliko ya ulimwengu na teknolojia,sasa yale mawazo ya vijiji vya ujamaa watu kuishi maporini na Azimio la Arusha yamepitiwa na wakati lazima Serikali walielewe hilo. Nimekuwa nikishangaa sana kuona Serikali ya Tanganyika inajaribu kufanya kila inavyowezekana kujaribu kuzuia na kuzima wimbi la Wazanzibar kupasua bahari na kuelekea Nchi kavu,kuna haja ya kujiuliza kulikoni ? Jee hii ni haki kwa nchi mbili zenye haki sawa na zilizoungana kwa hiari ?Mbona inaonekana zaidi kwamba Taifa moja linalitawala jengine. Muungano huu umekuwa ni ndoana kwa Wazanzibar na tusifikirie kwamba ndoana hii kwa vile tumeshaimeza tutakuwa salama hata tukiitoa basi lazima tushikamane. Watanzania lazima tukubali kwamba mabadiliko katika Muungano huu ni jambo la lazima kama kufa na mwanaadamu,tukidharau basi tukubali kwamba madhara yake yatakuwa makubwa kuliko faida yake. Wazanzibar wamechoka na utashi wa watu binafsi kujiona kwamba Zanzibar ni miliki ya kikundi fulani,watu fulani, chama fulani,fikra kama hizo zitatufikisha pabaya. Leo hii imekuwa ni mazoea kwa Serikali ya Tanganyika kuwanyanyasa Wazanzibar kwa kutumia vitimba kwiri na Wahafidhina wa Kizanzibar waliopandikizwa kuzima madai ya Wazanzibar kuhoji uhalali wa Muungano.Imekuwa kama desturi kwa Viongozi wa bara hasa wastaafu akina, Ali Hassan Mwinyi,Benjamini mkapa kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar lakini pia kuzidisha hasama miongoni mwa Wazanzibar, hali hii tutaenda nayo mpaka lini.Sio kweli kwamba wanawapenda Wazanzibar bali wanayafanya hayo kulinda maslahi yao binafsi.Wakati umefika kuachiwa Wazanzibar wajiamulie mambo yao wenyewe, na kuwa Taifa huru,hivi Watanganyika wanaogopa nini ? Muungano huu umekuwa kama ni chaka ambalo limeficha siri nzito,linalindwa kwa nguvu zote za dola lakini kubwa zaidi ni kuona hata waandishi wa habari kule bara wanashirikiana vizuri na Serikali yao ili kuisadia kuwakandamiza Wazanzibar kudai haki yao. Nimekuwepo Zanzibar kwa muda mrefu sasa, nimeona na kushuhudia mengi yanayotokea hapa Zanzibar lakini takribani waandishi wote wa habari wanashirikiana na vyombo vya dola kuficha ukweli na kuzidi kuwaona Wazanzibar kama vile ni maadui pale wanapodai haki yao ya msingi ndani ya Muungano.Nilifikiria kuona kama vyombo vya habari vitakuwa mstari wa mbele kufichua uovu katika jamii yetu kinyume chake ndio wao wanaoikandamiza Jamii yetu kwa fitna,uongo na ubabaishaji wa habari na matukio ya kweli.Fahari ya vyombo vya habari pamoja na waandishi waTanzania ni kutangaza propaganda za Serikali na jinsi ya kuwadhibiti Wananchi ili waone kwamba umaskini tulionao ndio maumbile yetu ,sasa hio demokrasi inayozungumziwa na katiba mpya inayotegemewa ipo wapi. Ukweli unafichwa na propaganda ndizo nyimbo za Waandishi wa habari na baadhi yao tayari wanafanya kazi ya serikali ya Tanganyika kupotosha wananchi na ulimwengu kwa jumla ukweli na uhalisia wake.Sasa taaluma hii ya uandishi ina maana gani kwa Watanzania,ikiwa yale maovu yaliotawala kwenye jamii yanashindwa kufichuliwa.Hii ni kutokana na serikali ya Tanganyika kuwarubuni kwa nia ya kuendeleza sera ambazo kwa ulimwengu huu tunaokwenda nao hazikubaliki tena. Ingawaje Serikali ya Tanganyika imejipanga vizuri kwa kupenyeza vibaraka wake ndani ya Zanzibar ambao huwalai kwa madaraka baadhi ya Viongozi ili iwe rahisi kwao kuwathibiti Wazanzibar ni vyema baadhi viongozi hawa wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakaelewa kwamba hivi sasa maji yameshamwagika,Wazanzibar wameshikamana kudai haki yao na hapana budi kuungana nao ili malengo ya Wazanzibar yafanikiwe kwa usalama na amani bila ya kumwaga damu.Ule wakati wa kugombea vyeo umeshapitiwa na wakati,huu nu wakati wakuona Kwamba Jamhuri ya watu Wazanzibar kwanza,baadae ndio tuangalie utawala na mstakabali wetu kwa pamoja. ZANZIBA KWANZA: source mzalendo.net

No comments:

Post a Comment