Thursday, June 28, 2012

pinda akwepa kujiuzulu

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema hawezi kujiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kutatua matatizo ya madaktari. Pinda amelieleza Bunge kuwa, hadhani kama ni busara kujiuzulu kwa sababu ya matatizo ya madaktari na kwamba suala hilo ni la muda mrefu na ni changamoto. Waziri Mkuu ametoa msimamo huo wakati anajibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ambaye alisema, kwa kuwa matatizo ya madaktari ni ya muda mrefu, na Pinda ameshindwa kuyamaliza, kwa nini asijiuzulu. Waziri Mkuu amelieleza Bunge kuwa, amefanya kila aliloweza kumaliza mgogoro kati ya Serikali na madaktari. Lissu alimuuliza Pinda kuwa, kama amefanya kila aliloweza kumaliza tatizo hilo na ameshindwa kwa nini asijiuzulu. Waziri Mkuu amemjibu kwamba, anamuheshimu sana, na hadhani kama hiyo ni namna nzuri ya kumuuliza. Spika wa Bunge, Anne Makinda, amefunga mjadala kuhusu mgogoro wa Serikali na madaktari kwa kuwa Mahakama imelalamika kwa kuwa, suala hilo lipo mahakamani lakini wabunge wameendelea kuuliza, kudadisi na kutoa taarifa. Kutokana na msimamo huo wa Bunge, Serikali leo haitatoa msimamo wake kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea katika hospitali nyijngi nchini zikiwemo hospitali za rufaa. Makinda ametoa msimamo huo wakati anatoa mwongozo alioomba Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye alimuomba aagize Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii itoe taarifa bungeni kuhusu waliyoyaona walipotembelea hospitali na kuzungumza Serikali, madaktari, na wadau wakati wa mgomo uliopita wa madaktari. Makinda amewaeleza wabunge kuwa, yeye ndiye aliyeituma kamati kufanya kazi hiyo, na ilitoa taarifa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi hivyo taarifa hiyo haitawasilishwa bungeni. “Sasa suala hili lipo mahakamani na huo mjadala umefungwa”amesema Makinda.

No comments:

Post a Comment