Thursday, August 11, 2011

AFYA YA KONDOO MWENYE QUR'AN MATATANI

AFYA ya kondoo wa ajabu
aliyezaliwa katika Kijiji cha Uduru
wilayani Hai mkoani Kilimanjaro
iko shakani kutokana na
mazingira yasiyo salama
anakoishi.
Bwana Mifugo wa vijiji vya Uduru
na Nkuu Andrea Njau amesema
jana kuwa kondoo huyo yupo
katika mazingira hatarishi ya
kuambukizwa magonjwa
yanayotishia maisha yake.
“Kondoo huyo yupo katika
mazingira ambayo hayastahili
hata kidogo, magonjwa kama ya
homa ya mapafu, ndigana baridi,
kimeta pamoja na fangasi
yatakuwa yakimnyemelea,”
alisema Njau.
Njau alisema tangu aanze
kuhudumia mifugo katika kijiji
hicho, hajawahi kutoa tiba wala
chanjo katika familia ya mmliki
wa kondoo huyo, Grace Masawe
hali inayotishia zaidi maisha ya
kiumbe huyo.
Akifafanua sababu na dalili za
magonjwa hayo yanayopatikana
katika kijiji hicho, Njau alisema
kuwa homa ya mapafu ambayo
husababishwa na minyoo ya
mapafu, mfugo huwa na homa
kali na hutoa mapovu mdomoni
na hatimaye kufa.
Kuhusu ugonjwa wa ndigana
baridi, Njau alisema
husababishwa na kupe
wanaozaliana kwa wingi
kutokana na kinyesi cha
ng'ombe na kuonya kuwa kama
kondoo huyo anakaa zizi moja
na ng’ombe, yuko hatarini
kuupata.
Ugonjwa mwingine hatari
unaomnyemelea kondoo huyo ni
kimeta (anthrax) ambao huua
mifugo ghafla pamoja na
binadamu.
Alisema ugonjwa huo uliwahi
kuzuka hivi karibuni katika eneo
hilo lakini ulidhibitiwa kwa
haraka kabla ya kuleta madhara
makubwa.
Ugonjwa wa kimeta hauna dawa
yoyote zaidi ya chanjo ambayo
katika Wilaya ya Hai mwanzoni
mwa Juni chanjo hiyo ilitolewa.
Alisema mbali na kutowahi
kuhudumia mifugo ya familia ya
Masawe, lakini hata wakati wa
chanjo dhidi ya kimeta, wafugaji
wachache walitoa mifugo yao
kutokana na kukosa elimu.
Masawe alikiri kuwa hajawahi
kupatia mifugo yake chanjo ya
aina yoyote hata na kondoo huyo
kwa madai kuwa hana fedha ya
kuwapatia matibabu.
Mmiliki huyo alisema kuwa katika
mifugo yake ulishawahi kuzuka
ugonjwa ambao hakuutambua
ukaua ng'ombe wake ghafla.
Kutokana na hali hiyo, Njau
alishauri jamii ijitokeze
kumsaidia mama huyo ili amlinde
kondoo huyo dhidi ya hatari ya
magonjwa.
Kondoo huyo dume alizaliwa
Julai 6 mwaka huu, akiwa na
maandishi ya Kiarabu ubavuni
yenye maana ya neno Yasini
ambayo ni aya muhimu sawa na
moyo wa Kitabu Kitakatifu cha
Koran.
Tangu aripotiwe na gazeti hili,
kondoo huyo amekuwa kivutio
kikubwa kwa watu hususani
waumini wa dini ya Kiislamu
wanaomiminika kwa wingi
kutoka mikoa mbalimbali
kushuhudia maajabu hayo.
Waumini hao baadhi wamefikia
hatua ya kutaka kumnunua kwa
Sh milioni 10 lakini wakakataliwa
na mmiliki huku baadhi ya
mashehe wakisema ni dalili za
kiama.
Tayari Baraza la Waislamu Mkoa
wa Kilimanjaro limeshatoa
maelezo kuwa kondoo huyo ni
jambo kubwa na hivyo
wanamuachia Mungu.

No comments:

Post a Comment