Wednesday, August 24, 2011

JAIRO Vs BUNGE

BUNGE jana lilisitisha kwa muda
shughuli zake za kawaida kujadili
hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi,
Philemon Luhanjo kumrejesha
kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, David Jairo
kabla ya Bunge kujadili Ripoti ya
uchunguzi ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Hatua hiyo imekuja siku moja
baada ya Luhanjo kukutana na
waandishi wa habari Dar es
Salaam juzi na kuutangazia
umma kwamba kutokana na
matokeo ya uchunguzi huo
kutomtia hatiani anaamuru Jairo
arejee ofisini mara moja.
“Kutokana na matokeo haya ya
uchunguzi wa awali, mimi kama
Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu
Mkuu Nishati na Madini, sitaweza
kuendelea na hatua ya pili ya
kumpa taarifa ya tuhuma.
Ninaamuru David Jairo arejee
kazini kuanzia siku ya Jumatano.”
Hata hivyo, uamuzi huo wa
Luhanjo jana uliamsha hasira za
wabunge bila kujali itikadi zao za
kisiasa ambao ambao walitaka
Bunge lisitishe kujadili shughuli
zozote kutokana na hatua hiyo
ya Katibu Mkuu Kiongozi
wakisema ni kudharau Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge.
Hoja ya Zitto
Hoja hiyo iliwasilishwa na
Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema) muda mfupi kabla ya
kuanza kwa kipindi cha maswali
na majibu. Zitto ambaye pia ni
Naibu Kiongozi wa Upinzani
Bungeni alitoa hoja kutaka
Bunge lisitishe kujadili hoja zote
za Serikali hadi hapo ripoti ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali iliyomsafisha
Jairo itakapofikishwa bungeni na
kujadiliwa.
Zitto alianzisha moto huo mnamo
saa 3:17 asubuhi ikiwa ni dakika
moja tu baada ya Naibu Spika,
Job Ndugai kutangaza taratibu za
safari ya wabunge kwenda
Zanzibar kwa ajili ya mazishi ya
Mbunge Mussa Khamis Silima
aliyefariki juzi.
Alitumia kanuni ya 51 kulieleza
Bunge kuwa kitendo
kilichofanywa na Luhanjo
kilikiuka haki, maadili na
madaraka ya Bunge na hivyo
akataka wabunge wenzake
wamuunge mkono ili wagome
kufanya shughuli zozote za
Serikali hadi hapo ripoti ya CAG
kuhusu tuhuma dhidi ya Jairo
itakapowasilishwa rasmi
bungeni.
“Mheshimiwa Naibu Spika, jana
kupitia vyombo vya habari
tulimsikia Katibu Mkuu Kiongozi
kupitia vyombo vya habari
akieleza kuwa tuhuma
zilizokuwa zikimkabili Jairo si za
kweli na kwamba anatakiwa
kurudi kazini kuanzia leo (jana),’’
alisema Zitto na kuongeza:
“Mheshimiwa Naibu Spika
unafahamu ya kwamba, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania alizungumza ndani
ya Bunge hili ya kwamba
angekuwa ni yeye
angeshamchukulia hatua Ndugu
Jairo kuhusu vitendo alivyofanya,
hivyo basi naomba nitoe hoja
kwamba Bunge lisitishe hoja
yoyote ya Serikali mpaka
itakapoleta bungeni taarifa ya
CAG kuhusiana na uchunguzi
huo.”
Baada ya kutoa hoja hiyo, Zitto
aliungwa mkono na wabunge
zaidi ya nusu waliokuwamo
ndani ya ukumbi, hali ambayo
ilimlazimisha Naibu Spika wa
Bunge, Ndugai, kuitisha Kamati
ya Uongozi kwa dharura kujadili
suala hilo.
Hoja ya Lukuvi
Baada ya hoja ya Zitto, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi
alisimama kupinga hoja hiyo
akisema Mbunge huyo hakufuata
taratibu zilizotakiwa ambazo ni
kuwasilisha kusudio kabla ya
kutoa hoja rasmi.
“Mheshimiwa Naibu Spika, najua
jambo hili lina public interest
(masilahi ya umma), lakini kanuni
zinasema kuwa mbunge
anayetaka kuwasilisha jambo
lolote linalohusiana na shughuli
za Bunge atafanya hivyo wakati
unaofaa na uliowekwa na kanuni
na atakuwa amemwarifu Spika
mapema kuhusu kusudio lake,
hivyo ulitakiwa kuwasilishiwa
mapema ili uweze kuamua,’’
alisema Lukuvi.
Akijibu hoja hiyo, Ndugai
alisema: “Wakati nasoma
matangazo mbalimbali
kuhusiana na kifo cha Mbunge,
nilipata taarifa kutoka kwa Zitto
kuhusu kunitaarifu juu ya jambo
hilo, hivyo basi, hoja iliyotolewa
na Zitto imetolewa kwa wakati
na ilifuata utaratibu unaotakiwa.’’
Uamuzi wa Kamati ya Uongozi
Baada ya kikao cha dharura cha
Kamati ya Uongozi ya Bunge,
ilipotimu saa 3:58, kabla ya
kumalizika kwa maswali na
majibu, Ndugai alirejea ukumbini
na kutoa taarifa kuwa kikao
hicho kiliongozwa Spika wa
Bunge, Anne Makinda na
kukubaliana na hoja ya Zitto.
“Kikao kilihudhuriwa na Spika
wa Bunge, Anne Makinda na
alikiendesha yeye mwenyewe.
Kamati imepima hoja iliyotolewa
na Zitto na kuona ni hoja
inayohitaji kusikilizwa na Bunge
na hakuna kipingamizi
chochote,” alisema Ndugai na
kushangiliwa kwa nguvu na
wabunge.
Baada ya hapo Naibu Spika
alimpa nafasi mtoa hoja, Zitto
kuanza kujadili hoja hiyo na
Mbunge huyo alisema jambo hilo
lilikuwa ni la aibu kubwa mbele
ya wabunge na taifa kwa ujumla.
“Jambo hili lilianzia bungeni na
hivyo ripoti hiyo ilipaswa kuanzia
humu bungeni. Kitendo cha
Katibu Mkuu Kiongozi ni dharau
kwa Bunge na kwa kuwa Waziri
Mkuu alisema anamsubiri Rais,
amemdharau na ninasema kama
ningekuwa mimi ni Waziri Mkuu
ningejiuzulu nafasi yangu mara
moja,’ ’alisema Zitto.
Zainabu Vullu
Mbunge wa pili kuchangia hoja
hiyo alikuwa Zainabu Vullu (Viti
Maalumu - CCM), alisema kitendo
hicho kinaudhi na kuwataka
wabunge kuungana akisema
madaraka yao yalikuwa
yameingiliwa.
“Nianze kwa kuangalia Katiba
kifungu namba 63 cha katiba
Ibara ya Pili ambayo inasema
sehemu ya pili ya Bunge itakuwa
ndiyo chombo kikuu cha Jamhuri
ya Muungano ambacho kitakuwa
na madaraka kwa niaba ya
wananchi kusimamia na
kuishauri Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na vyombo vyake
vyote katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa
katiba,” alisema Vullu na
kuongeza:
“Suala lile liliibuliwa ndani ya
Bunge hili na baada ya kuibuliwa,
Mheshimiwa Waziri Mkuu
ambaye naye ni mbunge
mwenzetu lilimgusa. Ni matarajio
yetu baada ya utafiti na
uchunguzi uliofanyika suala hili
lingerudi kwetu tukalijadili na
kuona nini kilichotokea na
kuhabarisha wananchi wetu ni
jinsi gani ya matumizi ya fedha
za nchi hii ambazo jasho la
wananchi zilivyotumika.”
Alisema kutokana na taarifa ya
Luhanjo, bunge ni kama
limedhalilishwa na kwamba
halikupewa haki yake kwani
wabunge wote wameonekana
kama watu wasiojua wajibu
wao.
Sendeka
Mjadala wa hoja hiyo
ulihitimishwa na mchangiaji wa
tatu, Mbunge wa Simanjiro (CCM),
Christopher Ole Sendeka ambaye
alikuja na hoja jingine ya
kuomba Bunge lipitishe azimio la
kuunda Kamati Teule
kuchunguza suala hilo. Hoja hiyo,
kama ilivyokuwa ile ya Zitto pia
iliungwa mkono na wabunge
karibu wote.
Sendeka alisema kitendo cha
Luhanjo kutangaza ripoti hiyo ni
kupoka nafasi ya Bunge na
kwamba Waziri Mkuu
amedharauliwa kwa kiasi
kikubwa.
“Ninaomba kutumia kanuni ya
117 kuliomba Bunge lako tukufu
sasa liamue kuunda kamati teule
itakayoangalia pamoja na
mambo mengine, kuingiliwa kwa
uhuru wa Bunge, lakini
mchakato mzima uliosababisha
fedha zote zile zikusanywe na
kugawanywa na kuitishwa kama
fedha za harusi wakati tunajua
kwamba kila waziri anapewa
kasma ya maandalizi ya bajeti
inayokuja,” alisema Sendeka na
kuongeza:
“Wote (watumishi) waliokuja
waliweza kuja na mafuta kutoka
katika ofisi zao naomba Bunge
hili, Mheshimiwa Naibu Spika
liniunge mkono kwa kutoa hoja
kwa mujibu wa kanuni ya 117,
fasili ya kwanza ya pili mpaka ya
nne ambayo inaweka masharti
ya kuundwa kwa kamati teule na
hii itasaidia sana kuitendea haki
hoja hii na kulinda hadhi ya
Bunge lako tukufu.”
Msimamo wa Bunge
Baada ya Sendeka kutoa hoja
hiyo, Ndugai alisimama na
kusema: “Sasa hoja hiyo
Mheshimiwa Ole - Sendeka
ameiboresha kwa kutoa hoja ya
kuunda tume teule ambayo
waheshimiwa wabunge
mmeiunga mkono kwa wingi
sana kwa kutumia kanuni ya 117
ambayo inasema kamati teule
inaweza kuundwa na Bunge kwa
madhumuni maalumu kwa hoja
mahsusi itakayotolewa na
kuafikiwa.”
“Mimi ninakubaliana na jambo
hili na kwa jinsi hiyo, kufuatana
na kanuni hiyo ya 117 Bunge hili
litaunda tume teule kwa ajili ya
kulichunguza jambo hili kwa
sababu Bunge ni mhimili,
haliwezi kudharaulika kiraisi na
tunaiheshimu na kuipenda sana
Serikali yetu inayoongozwa na
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete
na Waziri mkuu wake Mizengo
Pinda.”
“Si rahisi kwa Bunge kuonekana
Waziri Mkuu akidharaulika
likanyamaza! Haiwezekani, kama
dharau inaweza kutokea
hukohuko si ndani ya Bunge
hili.”
Baada ya uamuzi huo, Mbunge
wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod
Mkono alijaribu kupinga uamuzi
huo akitaka jambo hilo liende
kwa utaratibu ili Bunge lisije
likaingilia taratibu za mihimili
mingine. Alihoji kwa kitendo cha
kutompatia nafasi Jairo ili ajieleze
lakini Ndugai alisema jambo hilo
alishalifunga lakini akamtoa
shaka mbunge kuhusu haki:
“Kama ni kuhojiwa basi ataitwa
akahojiwe huko asipotendewa
haki hiyo utaleta hoja yako.’.
Jairo apokewa kishujaa
Wakati wabunge
wakimng'ang'ania, Jairo
alipokewa kwa mbwembwe
aliporipoti ofisini kwake Dar es
Salaam huku baadhi ya
wafanyakazi wakisukuma gari
lake na kuimba: “Baba, baba
baba huyooo, karibu baba,
karibu baba, umeshinda vita
karibu nyumbani.’
Akizungumza baada ya kuingia
ofisini, Jairo alisema:
“Nimesamehe kwa upendo
mkubwa. Siwezi kulipiza kisasi,
wala sitachukua hatua zozote
kwa kuwa mimi ni Mkristo
nimerudi kwa amani, tuchape
kazi tujenge nidhamu,” alisema.
Mara baada ya kufika ofisini
kwake, Jairo akionekana
mwenye uso uliojaa furaha huku
akilengwa na machozi alisimama
mbele ya kiti chake akiwa kimya
akitazama chini na kisha alitoka
na kuelekea ofisini kwa Waziri
wake, William Ngeleja.
“Nimejipanga kuchapa kazi kwa
bidii na kudumisha ushirikiano
uliokuwapo tangu awali,
nashukuru haki imetendeka na
sitawashtaki wale
walionituhumu,’’ alisema Jairo na
kuongeza kwamba watu
wajielekeze kwenye mambo ya
maendeleo kuliko kufuatilia mtu
mmojammoja, kwa kuingiza
maslahi binafsi.
Waziri Ngeleja alisema
ameshukuru kwamba Jairo
amerudi baada ya misukosuko ya
hapa na pale.
LHRC wapinga
Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) kimepinga
hatua ya Serikali kumsafisha Jairo
na kisha kumtaka arejee kazini,
kikisema hatua hiyo
imedhalilisha Bunge.
“Taarifa ya kusafishwa kwa Jairo
inaashiria mambo matatu,
kwanza inaonyesha kuna
mkakati wa kuwalinda viongozi
pale wanapofanya makosa. Pili,
taarifa hiyo imelidhalilisha Bunge
ambalo ndilo lilifichua kashfa
hiyo, Beatrice Shelukindo ndiye
aliyefichua hayo. Tatu, taarifa
hiyo imemdhalilisha Waziri Mkuu
na kumfanya aonekane
kutokuwa makini na kauli zake
hasa pale aliposema kuwa
angeweza kumchukulia hatua
Jairo lakini anasubiri taarifa ya
Rais.”
Policy Forum yakosoa
Mratibu asasi ya kiraia ya Policy
Forum, Semkae Kilonzo alisema
Serikali imechukua uamuzi huo
bila ya kuzingatia uzito wa jambo
husika. Alisema umefika wakati
iache kufanya kazi kwa mazoea
na iheshimu mamlaka ya mihimili
mingine.
Alisema Katiba ya sasa katika
Ibara ya 63, kifungu kidogo cha
1 hadi 3 inaeleza bayana,
mamlaka ya Bunge na kusisitiza
kuna haja ya mhimili huo
kupewa meno zaidi kwa mujibu
wa sheria ili ushauri na maoni
yake yaweze kutekelezeka.
“Wabunge walishaeleza maoni
yao kuhusu sakata hilo lakini
serikali imechukua hatua bila ya
kuzingatia uzito wa jambo
lenyewe, cha msingi hapa ni
bunge liongezewe meno zaidi ili
kazi zake ziweze kuheshimika na
kutekelezeka,” alisema Kilonzo.

No comments:

Post a Comment