Friday, August 5, 2011

NJAA YAZIDI KUIANDAMA SOMALIA

Umoja wa Mataifa unasema
maeneo matatu zaidi ya Somalia
sasa yanakabiliwa na njaa.Ripoti
zinasema kuwa njaa inatarajiwa
kuenea zaidi kama hakuna
uingiliaji kati wa haraka.
kitengo cha Umoja wa Mataifa
cha tathmini ya usalama wa
chakula na mradi wa kuonya juu
ya njaa ujulikanao kama FEWS-
NET unasema njaa huko kusini
mwa Somalia inazidi kuwa
mbaya.
Takwimu mpya zinaonyesha
kwamba watu zaidi wanafariki
na kuathiriwa na hali mbaya ya
utapiamlo katika mkoa wa Middle
Shebele na pia miongoni mwa
watu waliopoteza makazi yao
huko Mogadishu na eneo la
Afgoye magharibi mwa mji
mkuu.
Hadi sasa hali ya njaa
imetambuliwa katika maeneo
mawili tu ya Lower Shebelle na
Bakool kusini mwa kati ya
Somalia.
Mshauri mkuu wa masuala ya
kiufundi katika kitengo cha
usalama wa chakula kwa somalia
katika Umoja wa Mataifa, Grainne
Maloney anasema hali katika
jamii za watu waliopoteza
makazi yao ni za kusikitisha.
“Ni kundi ambalo kwa kiasi
kikubwa tayari limekoseshwa
makazi na walikuwa
wakitegemea misaada ya
kibinadamu, na bila shaka
kukiwa na masharti katika
kuwafikia na masharti katika
ufadhili, hawakuweza kupata
msaada. Takriban miaka 3
iliyopita kiwango cha utapiamlo
huko kilikuwa takriban asilimia
12 na kuona hivi sasa kiwango
hicho kimefikia asilimia 40
inasikitisha.”
Hali ya njaa kimsingi hivi sasa
inamaanisha kuwa takriban
asilimia 30 ya raia wana
utapiamlo, watu majumbani
hawana fursa ya kupata chakula
na kwamba vifo vimetokea
kutokana na njaa.
Hakuna takwimu halisi kuhusu
idadi ya vifo vinavyotokea kila
siku,lakini inakadiriwa kuwa ni
mamia ya watu.
Umoja wa Mataifa imeomba
msaada wa zaidi ya dola billion
moja kushughulikia mzozo na
hadi sasa wamepata takriban
asilimia 40 ya fedha hizo
zilizoombwa. Maloney anasema
msaada zaidi unahitajika haraka.
“Kuna haja ya uingiliaji kati
mkubwa hivi sasa kwa vile sasa
watu millioni 2.8 huko kusini
wanahitaji msaada na hiyo ni
pamoja na chakula, lishe bora,
maji, afya na vifaa vya kilimo.
Wanahitaji kila kitu hivi sasa na
hawawezi kusubiri.”
Maloney anasema kuna
matumaini kidogo kwa
Mogadishu, ambako watu
waliopoteza makazi yao
wanaweza kufikiwa na
mashirika ya misaada ya
kibinadam ambayo yanapanua
juhudi zao huko.
Mzozo wa Somalia ulisababishwa
na mkongo mbaya wa ukame,
ambao baadhi wanasema ni
mbaya zaidi kuwahi kufanyika
katika miaka 60. Lakini ukosefu
wa kuwepo serikali inayofanya
kazi vilivyo imeifanya hali hiyo
kuwa mbaya zaidi na vikwazo
vya misaada vilivyowekwa na
kundi la Al shabab lenye
uhusiano na kundi la kigaidi la Al
Qaida.
Umoja wa Mataifa unategemea
njaa kuenea katika maeneo
mengine ya kusini mwa Somalia
katika majuma manne au sita
yajayo na kuendelea hadi mwezi
Disemba.

No comments:

Post a Comment