Wednesday, August 10, 2011

BAKWATA KUTOLEA TAMKO KONDOO MWENYE KORAN

BARAZA Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata) Mkoa wa
Kilimanjaro, linatarajia kutoa
tamko lake juu ya kondoo
aliyezaliwa akiwa na maandishi
ya Koran.
Hayo yalisemwa jana na Katibu
wa Bakwata wa Mkoa, Shehe
Rashid Malya, alipozungumza na
gazeti hili baada ya kikao
kilichokuwa kitoe tamko hilo
jana kuahirishwa.
Kuahirishwa huko kulitokana na
Shehe wa Mkoa ambaye alikuwa
asimamie kikao hicho kushindwa
kufanya hivyo, kutokana na
sababu zilizokuwa nje ya uwezo
wake.
Awali ilibainishwa kuwa
mashehe wa mkoa huo
walikuwa wakutane wajadili
kuhusu kondoo huyo na kisha
kumpa tamko Shehe wa Mkoa na
kuliwasilisha kwa jopo la wasomi
ambao ndio wangetoa tamko
rasmi kuhusu majaaliwa hayo.
Kondoo huyo aliyezaliwa Julai 6
amekuwa kivutio kikubwa kwa
waumini wa dini ya Kiislamu,
ambapo hadi sasa watu kutoka
mikoa ya Dar es Saalam, Tanga na
Arusha wamefika kushuhudia
maajabu hayo.
Hadi sasa pamoja na watu
kumiminika katika kijiji cha
Uduru wilayani Hai
kumshuhudia, kuna watu
wamejitokeza kutaka kumnunua
kwa hata Sh milioni 10 lakini
mmiliki wake, Grace Masawe,
anasema hayuko tayari
kumwuza.
Alieleza sababu za kukataa
kumwuza kondoo huyo, kuwa ni
kutokana na familia yake kutojua
nini maana ya tukio hilo na
kwamba inachukulia kitendo
hicho kama baraka kwa familia.
Maandishi aliyonayo kondoo
huyo yana maana ya Yasini
ambayo ni moja ya aya muhimu
katika Koran pia ni moyo wa
Kitabu hicho.
“Aya hii ni moyo wa Kitabu
Kitakatifu cha Koran,
kinachoelezea mambo mengi
makubwa hususani nyakati za
mwisho … inaonesha ishara
kuwa hizi ni siku za mwisho za
kiyama,” alisema Shehe Malya.
Alisema aya ya maandishi hayo
katika Koran ni moja ya sura
zinazoeleza mambo mazito,
pamoja na kueleza kuwa Kitabu
hicho kinazungumzia siku za
mwisho za kiyama, hivyo kila mtu
atengeneze maisha yake.
Aliongeza kuwa hiyo ni ishara
kubwa kwa waumini wa dini ya
Kiislamu, kwa sababu Kitabu
Kitakatifu cha Koran kilishushwa
Mwezi wa Ramadhan, hivyo
ishara hii katika kipindi cha
Mfungo Mtukufu wa Ramadhani
ni kubwa.
Pia Shehe Malya aliongeza kuwa
neno Yasini ni jina lingine la
Mtume Muhammad (SAW)
alilopewa na Mwenyezi Mungu,
na kueleza kuwa hiyo ni miujiza
na bahati kwa dini hiyo.
“Haya maandishi katika aya ya
Kitabu cha Koran yamejikita zaidi
kuonesha hizi ni siku za mwisho
za kiyama, hivyo wakati huo
midomo haitaongea tena ila
mikono itasema na miguu
itashuhudia, hivyo Mungu
akipenda jambo lake liwe
linakuwa,” alisema Shehe Malya.
Grace alisema familia inayomiliki
kondoo huyo ni ya Kikristo,
ingawa ameibuka mmoja wa
wanafamilia, Said Masawe na
kusema si kweli kwamba familia
hiyo ni ya Kikristo bali ni
mchanganyiko wa Wakristo na
Waislamu.
Akizungumza na gazeti hili kwa
njia ya simu juzi, Masawe alisema
hatua ya kusema kuwa familia
hiyo ni ya Kikristo pekee,
imesababisha manung’uniko
ndani ya familia kwa vile
haijawatendea haki wanafamilia
Waislamu.
“Familia yetu ni ya mchanganyiko
wa dini mbili za Uislamu na
Ukristo. Pale nyumbani alipo yule
kondoo, mwenye mji ni
marehemu babu yetu Mzee Said
Masawe, ambaye mimi ndiye
nilirithi jina lake. Babu alikuwa
Mwislamu na hata marehemu
mkewe, yaani bibi pia alikuwa
Mwislamu jina lake ni Mwanaidi
Masawe.
“Si hao tu, hata baba mkubwa
Khalifa Masawe anayeishi
Monduli ambaye alikuwa pale
nyumbani, baada ya kuzaliwa
kwa kondoo yule, ni Mwislamu.
Alikuwapo pia marehemu baba
yetu mkubwa marehemu
Suleiman Masawe, ambaye ni
Mwislamu. Ninachotaka kusema
hapa ni kwamba Waislamu ndani
ya familia tupo wengi tu ingawa
na Wakristo pia wapo,” alisema
Masawe.
Alisema mama yake anayeishi
katika makazi hayo kwa hivi sasa
ambaye ndiye aliyelieleza gazeti
hili, kuwa familia yao ni ya
Kikristo, Grace (55), alizungumzia
imani yake yeye binafsi, kwani ni
Mkristo, lakini hiyo haina maana
kuwa wanafamilia wote ni
Wakristo.
“Hivi sasa baada ya tukio, baba
mkubwa (Khalifa), ametutaarifu
wanafamilia wote lakini kwa vile
tukio limetokea wakati wa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani,
tumekubaliana kwamba baada
ya funga, wakati wa Sikukuu ya
Idd wote tuwe Moshi ili tusome
dua na kumaliza kila kitu kwa
jambo hili la ajabu lililotokea,”
alisema Masawe.

No comments:

Post a Comment