Thursday, June 23, 2011

BEI YA MAFUTA YA TAA KUPANDA MARA 7

MAFUTA ya taa na maji ya
kunywa ya chupa yatapanda bei
kutokana na uamuzi wa Serikali
kupandisha ushuru wa bidhaa
hizo.
Kupanda kwa mafuta ya taa ni
dhahiri kutawasononesha
Watanzania wengi hasa vijijini,
lakini Serikali imejitetea kuwa
uamuzi huo umechukuliwa ili
kuepukana na uchakachuaji
mafuta, ambao umeelezwa kuwa
unaididimiza nchi kiuchumi.
Akiwasilisha Muswada wa Sheria
ya Fedha mwaka 2011, Naibu
Waziri wa Fedha, Pereira Silima,
alisema jana kuwa Serikali
imeongeza ushuru wa bidhaa
kwa mafuta ya taa kutoka Sh 52
hadi Sh 400.30.
Uamuzi huo unaondoa tofauti
iliyokuwapo kati ya bei ya dizeli
na bei ya mafuta ya taa na pia
utadhibiti uchakachuaji wa dizeli
ambao hufanywa na
wafanyabiashara kwa
kuchanganya dizeli na mafuta ya
taa, ili kujipatia faida kubwa, kwa
kuwa kodi au bei kwenye mafuta
ya taa ni ndogo.
Eneo hilo la kupandisha bei ya
mafuta ya taa lilipokewa kwa
hisia tofauti na wabunge
ambapo Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge (CCM)
alipongeza hatua hiyo kwa
maelezo kuwa bei ndogo ya
mafuta hayo ilikuwa inanufaisha
watu wachache hasa
wafanyabiashara.
Lakini Mbunge wa Mbozi
Mashariki, Godfrey Zambi (CCM),
alitaka Serikali isipandishe
ushuru wa mafuta ya taa, kwani
ndiyo yanategemewa na
wananchi wengi vijijini.
Amesema, kisingizio cha
kupandisha ushuru huo kwa
kuogopa wachakachuaji,
kinaonesha dhahiri kuwa Serikali
imeshindwa kuwadhibiti
wachakachuaji hao.
Kwa upande wa maji ya kunywa
ya chupa, kinywaji hicho
kimewekwa kwenye kundi la
vinywaji baridi ambavyo ushuru
wake utapanda kutoka Sh. 63,
hadi Sh. 69 kwa lita. Uamuzi huo
utapandisha bei ya maji ya
kunywa ya chupa kama ilivyo
kwa soda na juisi.
Eneo hilo lilipata upinzani kutoka
kwa wabunge, akiwamo
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha
na Uchumi, Dk. Abdallah Kigoda,
ambaye wakati akiwasilisha
maoni ya Kamati hiyo, alisema
maji ya kunywa ya chupa
yasiongezwe ushuru.
“Tunaishauri Serikali kutoongeza
ushuru kwa bidhaa hizo, kwani
yanatumika na wananchi wengi
wa vijijini na mijini … ni bidhaa
muhimu na ya lazima,” alisema
Kigoda.
Dk. Kigoda amesema, bidhaa hiyo
ya maji imesaidia kupunguza
maambukizi yaliyokuwa
yakisababishwa na maji yasiyo
salama katika baadhi ya maeneo
nchini.
Chenge katika eneo hilo, alisema
maji ya chupa kutokana na
kuuzwa bei ya chini wananchi
wengi wa vijijini wanayatumia
na kupunguza magonjwa ya
kuhara, hivyo yasiongezwe
ushuru.
Katika Muswada huo wa fedha,
Serikali pia imepunguza kwa
kiwango cha asilimia 50 tozo za
mamlaka mbalimbali, ikiwamo
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Maji na Nishati (EWURA),
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri
wa Nchi kavu na Majini (Sumatra)
na Shirika la Viwango (TBS)
kwenye bidhaa za mafuta.
Amesema, kwa upande wa tozo
za aina hiyo zinazotozwa na
taasisi zingine kama Shirika la
Kusafisha Mafuta (Tiper),
Mamlaka ya Mapato (TRA) na
Mamlaka ya Bandari (TPA), Silima
alisema mikataba na hati husika
zitafanyiwa marekebisho ili
kutekeleza hatua hiyo ya Serikali
ya kupunguzo tozo hiyo kwa
asilimia 50.
Pia alisema ushuru wa mafuta ya
petroli kwa sasa na tozo zote
zitalipwa kwa kutumia sarafu ya
Tanzania au fedha za kigeni
zinazoweza kubadilishwa katika
shilingi ya kitanzania, ambayo
kwa mujibu wa utaratibu wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
malipo hayo yanaruhusiwa kwa
dola ya Marekani pekee.
Kuhusu kiwango cha faini ya
makosa ya usalama barabarani,
Serikali imepunguza kiwango
hicho kutoka Sh. 50,000 ya awali
hadi Sh. 30,000.
Amesema lengo la hatua hiyo ni
kuongeza adhabu kwa
watakaovunja sheria za
barabarani, ili kupunguza
ongezeko la ajali.
Hata hivyo, kiwango hicho
kiliendelea kupingwa na
wabunge na kambi ya Upinzani
ikitaka kiwango cha awali cha Sh.
20,000 kiendelee kwani Sh.
30,000 ni kubwa. Nayo Kamati ya
Fedha na Uchumi ilipinga kiasi
hicho na kutaka kishuke hadi Sh.
25,000.

No comments:

Post a Comment