Thursday, June 23, 2011

TATIZO LA MISHAHARA KWA WALIMU KUISHA MWAKANI

KUANZIA mwaka ujao wa fedha,
walimu wa shule za msingi na
sekondari hawatapata tena
matatizo ya kupata mishahara
mara wanaporipoti kazini.
Katibu Mkuu wa Tamisemi,
Hussein Kattanga amesema,
mwaka huu yametokea matatizo
ambayo yalisababisha baadhi ya
walimu kushindwa kulipwa
mapema mishahara yao ndio
maana yakatokea matatizo hayo.
“Tumejipanga kuhakikisha kuwa
mwalimu anaporipoti katika
kituo chake cha kazi analipwa
stahili zake zote,” amesema
Kattanga.
Amesema, wakurugenzi
watendaji watapelekewa fedha
hizo haraka na kwenye mfumo
wao wa malipo utakuwa
umeunganishwa moja kwa moja
Wizara ya Utumishi pamoja na
Fedha.
Alikuwa akizungumza kuhusu
maadhimisho ya Siku ya Serikali
za Mitaa mwaka 2011 ambayo
kitaifa yatafanyika mkoani
Rukwa Julai mosi mwaka huu na
mgeni rasmi atakuwa Waziri
Mkuu Mizengo Pinda.
Alisema, maadhimisho hayo
yatazinduliwa leo na Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa, Daniel ole
Njoolay mjini Sumbawanga.
Alifafanua kuwa lengo la Serikali
kugatua madaraka na kuziweka
shule hizo kwenye ngazi ya
halmashauri ni kutaka kutatua
matatizo kama hayo ya walimu
kwa haraka.
Alisema, licha ya sherehe ya
kitaifa kufanyika Sumbawanga,
lakini kila halmashauri itafanya
sherehe hizo katika eneo lao ili
kutoa fursa ya wananchi wa
maeneo husika kwenda kutoa
kero zao.
Alitoa mwito kwa wananchi
kujitokeza kwa wingi katika
maeneo ambako sherehe hizo
zitafanyika ili waelimishwe haki
zao na majukumu ya Serikali za
Mitaa.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya
mwaka huu ni mafanikio ya
Serikali za Mitaa katika miaka 50
ya Uhuru yatumike kuimarisha
ugatuaji wa madaraka kwa
wananchi kwa maendeleo yao.
Alisema, Serikali iliamua kutenga
siku maalumu kuadhimisha
sherehe hizo kila mwaka ili
kuwahabarisha wananchi juu ya
umuhimu wa serikali za mitaa,
nafasi na wajibu wao kwa
serikali za mitaa, pia kuwahimiza
wananchi kuhusu utekelezaji wa
shughuli za maendeleo kwa
lengo la kuchochea ukuaji wa
uchumi na kupunguza umasikini.
Alisema Siku ya Serikali za Mitaa
inatoa fursa kwa kila
halmashauri kuonesha shughuli
mbalimbali zinazotekelezwa
katika mamlaka zao.

No comments:

Post a Comment