Wednesday, August 8, 2012

Marekani yataka Rwanda kusitisha Msaada kwa Waasi wa M23

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton ameitaka serikali ya Rwanda kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kuwanyang'anya silaha waasi wa M23 na kusitisha msaada kwa Kundi hilo kwa lengo la kupata suluhu ya mgogoro wa Mashariki mwa nchi hiyo. Clinton amesema wanataka kuona nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR zinashiriki kikamilifu katika kurejesha usalama nchini DRC na kulisambaratisha Kundi la Waasi la M23 ambalo linatekeleza mashambulizi Mashariki mwa nchi hiyo. Kauli hii inakuja kipindi hiki ambacho Viongozi kutoka nchi kumi na moja za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakiwa kwenye mkutano wa siku mbili nchini Uganda kujadili usalama wa DRC ili kulimaliza Kundi la M23. Clinton ametaka Viongozi hao wa Ukanda wa Maziwa Makuu kutathimini kwa kina namna ya kuweza kushughulikia mgogoro huo na hatimaye kurejesha utulivu ambao umepotea Mashariki mwa DRC. Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu ICGLR umeingia siku ya pili ambapo Rais wa DRC Joseph Kabila Kabange hatukutana tena na Rais wa Rwanda Paul Kagame kama ambavyo ilipangwa awali na badala yake wataandaliwa kikao chao pekee. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Oriem Okello amesema Viongozi hao wawili hatokutana na badala yake Rais Yoweri Kaguta Museveni ataandaa mkutano baina yao na kwa sasa wamejiegemeza kujadili kupata Jeshi litakalolinda amani mpaka mwa DRC. Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu ICGLR wataamua Kikosi ambacho kitaenda kulinda mipaka ya DRC na kukabiliana na uasi ambao unafanywa na Kundi la Waasi la M23 ili kusaidia juhudi za amani. DRC yenyewe imeshaainisha haitaki nchi ya Rwanda ishirikishwe kwenye Jeshi hilo kutokana na kudaiwa kuwafadhili Waasi wa M23 huku Kigali yenyewe ikishinikiza inataka kushiriki kwenye mpango wa kurejesga amani. Katika hatua nyingine Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA Valerie Amos anaendelea na ziara yake kuangalia madhara ya mashambulizi ya Kundi la M23 nchini DRC. Amos amesema hali ni mbaya Jimboni Kivu kitu ambacho kama hakijadhibitiwa kinaweza kuzua maafa zaidi kwa wananchi wa eneo hilo kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakifanywa na Kundi la Waasi la M23. Kundi la Waasi la M23 limeendelea kujigamba kupiga hatua kwenye mapambano yake na Jeshi la Serikali hasa katika maeneo ya Rutchuru na sasa wanaendelea kusaka uungwaji mkono kutoka kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment