Sunday, August 12, 2012

ULIMBOKA AREJEA NCHINI AKIWA FITI

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka amerejea nchini jana akitokea Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu na kusema amepona kabisa. Ulimboka, ambaye alikuwa anaratibu migomo ya madaktari iliyofanyika mara mbili mfululizo, alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatano ya Juni 27, mwaka huu na kupelekwa katika msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ambako aliteswa na kujeruhiwa vibaya. Katika tukio hilo, daktari huyo aling’olewa meno mawili na kucha za mkono mmoja na baadaye kulazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya, Juni 30, mwaka huu, alisafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya vipimo na matibabu. Dk Ulimboka aliwasili jana saa nane mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitembea mwenyewe na kulakiwa na mamia ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam, wakiwamo madaktari wenzake pamoja na wanaharakati. Huku akibubujikwa na machozi pamoja na ndugu zake, madaktari na wanaharakati nao walimpokea kwa machozi kisha walimkinga kiasi ambacho kulitokea vurugu za kila mmoja kutaka kumwona. Akizungumza kwa ujasiri huku akizongwa na madaktari pamoja na wanahabari, Ulimbona alianza kwa kuwashukuru wote waliofika kumpokea na pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufikisha katika hali aliyonayo sasa pamoja na Chama cha Madaktari waliosaidia kupata fedha za matibabu. Alisema kwa sasa afya yake imeimarika na amepona kabisa na yuko tayari kufanya jambo lolote bila utata na kuruhusu maswali kwa wanahabari, lakini madaktari wenzake walikataa na kumtaka aende kwenye gari ili aondoke kwenda kupumzika. Alitii agizo hilo na kuondoka kwenda kwenye gari. Awali, kabla Dk Ulimboka hajawasili JNIA, nje ya uwanja wa ndege madaktari pamoja na wanaharakati walisikika wakiimba nyimbo mbalimbali zikiwamo za ‘Tanzania Nakupenda, ‘Kama siyo juhudi zako Nyerere’ pamoja na kuhamasishana kuwa Solidarity Forever (Mshikamano Daima). Baada ya kutembea hatua chache na kufika lilipokuwa gari lililombeba, Dk Ulimboka alisimama na kutaka kuzungumza jambo na wanahabari, lakini madaktari na nduguze walimkataza tena na kudai wamuache ili aende kupumzika. Katibu wa Jumuiya hiyo ya Madaktari, Dk Edwin Chitage akizungumzia gharama za matibabu ya Dk Ulimboka, alisema wanazikusanya na kujumlisha na watazieleza hivi karibuni kwa vyombo vya habari. Wanaharakati waliokuwapo uwanjani hapo, walizungumzia kurejea kwa Dk Ulimboka na kudai mapambano yameanza upya, kwani kilichomfanya daktari huyo kupigwa ni kupigania maslahi ya Watanzania wote. Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya alisema umefika wakati wa Watanzania kusimama na kuacha woga na unafiki katika kupigania haki za afya zao. Nkya alisisitiza kuwa mapambano aliyoyaanzisha Dk Ulimboka yanaendelea. Jambo lililoungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Malya alisema mapambano ya Dk Ulimboka ni ya Watanzania wote, hivyo kila mmoja anatakiwa kumuunga mkono. Dk Ulimboka alitekwa na kuumizwa vibaya wakati mgomo wa madaktari nchini ukiwa unaendelea, na tangu wakati huo baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani, na wanaharakati wamekuwa wakiituhumu Serikali kuhusika katika kutekwa na kupigwa kwa daktari huyo. Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mara kadhaa baada ya tukio hilo, imesisitiza kuwa haihusiki na unyama huo, na wala haikuwa na sababu ya kufanya hivyo. Tayari raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akituhumiwa kumteka na kufanya jaribio la kumwua Dk Ulimboka.

No comments:

Post a Comment