Sunday, August 12, 2012

Waislamu wa Myanmar wazidikuteseka

Ripoti mbalimbali kutoka Myanmar zinasema kuwa maafa makubwa yanatokea katika kambi ya wakimbizi wa Kiislamu katika jimbo la Rakhine. Kanali ya televisheni ya Press imeripoti kuwa watu karibu 20 wakiwemo watoto wadogo wamefariki dunia katika kambi hiyo ya Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Myanmar kutokana na ukosefu wa dawa na chakula. Ripoti hiyo inasema vijiji kadhaa vya Waislamu wa kaskazini magharibi mwa Myanmar vimeteketezwa kwa moto na Mabudha wanaosaidiwa na jeshi la polisi, na wakazi wa vijiji hivyo wamelazimika kuwa wakimbizi. Mabudha hao wenye misimamo mikali pia wamechoma moto misikiti kadhaa. Umoja wa Mataifa umesema kuwa ukatili wanaofanyiwa Waislamu wa Myanmar ndiyo mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani katika siku za hivi karibuni. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema kuwa jeshi la Myanmar limetenda jinai nyingi dhidi ya Waislamu wa Rohingya walio wachache. Ripoti hiyo imefafanua kuwa miongoni mwa jinai hizo ni kubakwa wanawake wa jamii hiyo ya Waislamu kaskazini mwa Myanmar.

No comments:

Post a Comment