Sunday, August 12, 2012

MJUSI ALIYEPELEKWA UJERUMANI KUREJESHWA NCHINI

SERIKALI ina mpango wa kumrudisha nchini mjusi maarufu aina ya Dinosaur aliyechukuliwa mkoani Lindi zaidi ya miaka 100 iliyopita na kupelekwa Ujerumani anakokadiriwa kuiingizia nchi hiyo zaidi ya Dola za Marekani bilioni tatu kwa mwaka, sawa na karibu Sh trilioni tano. Hayo yalisemwa bungeni juzi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alipozungumzia mikakati ya serikali katika kukuza utalii nchini. Nyalandu alisema Serikali itazungumza na Serikali ya Ujerumani juu ya suala hilo na kwamba, kama atarudishwa, atapelekwa mkoani Lindi. Aidha, alisema kama hilo litashindikana wataangalia pia uwezekano wa kupata asilimia fulani ya fedha inayotokana na watalii wanaomiminika kumuona mjusi huyo. “Katika mambo ya Kale, kuna hili la Mjusi wetu maarufu kama Dinasour ambaye taarifa tulizonazo anaipatia Ujerumani dola bilioni tatu kwa mwaka… huyu alichukuliwa Lindi na wakoloni wa Ujerumani akapelekwa iliyokuwa Berlin Mashariki… tunataka tumrudishe nchini, tutazungumza na Ujerumani… “Lakini niwahakikishie wabunge na Watanzania, tutawashirikisha wadau ili tujue sera na mtazamo wetu kama taifa kuona tutakavyoamua kuzungumza na Ujerumani tuamue kuomba mjusi wetu arudi tumweke Lindi au abaki huko huko, lakini tugawane mapato,” alisema. Masalia ya mifupa ya mjusi huyo, yalipatikana mwaka 1912 huko Tendaguru, Kata ya Mipango katika Jimbo la Mchinga, mkoani Lindi. Amehifadhiwa katika Makumbusho ya Humbolt huko Ujerumani. Nyalandu alikiri kuwapo kwa changamoto nyingi katika kukuza utalii, lakini Serikali imejipanga kufanya kazi kwa kasi ili kuhakikisha yanafanyika mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii ili ulinufaishe taifa. Alisema “Hali ya utalii nchini hairidhishi na wizara yangu imeazimia kufanya mabadiliko makubwa. Nchi yetu inapata watalii wachache tofauti na fursa tulizonazo. Dhamira ya Serikali ni kuona nchi inapata watalii milioni mbili kwa mwaka ifikapo mwaka 2015. Kwa sasa, watalii hawafiki milioni moja kwa mwaka.” Alisema mikakati hiyo itakwenda sambamba na kuongeza kasi ya ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni ili kuwa na uhakika wageni watakaokuja nchini hawakosi makazi. Nyalandu alisema mikakati pia inafanywa kuboresha mazingira ya viwanja vya ndege, akitolea mfano Uwanja wa Ndege wa Mwanza utapandishwa hadhi na mpango wa kuufanya kuwa wa kimataifa zaidi, utabadilishwa jina na kuitwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti.

No comments:

Post a Comment