Friday, September 27, 2013

Msanii Ahukumiwa Miezi Sita Kwa Kuimba Matusi

Msanii wa kizazi kipya nchini Tunisia, Ahmed Ben Ahmed, anayejulikana kwa jina la kiusanii, Klay BBJ, amehukumiwa jela kwa miezi sita kwa kuwatusi maafisa wakuu kupitia kwa muziki wake. Mahakama ilitupilia mbali kesi yake ya rufaa baada ya yeye na mwanamuziki mwenzake kupatikana na hatia mwezi jana ya kuwatusi maafisa wakuu katika tamasha la muziki eneo la Hammamet. Wawili hao awali walihukumiwa bila ya wao kuwepo mahakamani kutumikia kifungo cha miezi 21 lakini hukumu hiyo iliondolewa. Weld El 15, aliyepatikana na kosa kwa kuimba wimbo wake huo, kuwa 'Ploisi ni Mbwa', hakukata rufaa na sasa yuko mbioni. Hata hivyo Kaly BBJ lisema kuwa wimbo wao ulikuwa unaelezea hali ilivyo nchini Tunisia na kuhusu serikali. Muungano wa vyama unaoongozwa na chama cha wanasiasa waisilamu wenye msimamo wa kadri, Ennahda, uliingia mamlakani baada ya mapinduzi ya kiraia yaliyomwondoa mamlakani aliyekuwa rais Zine el-Abidine Ben Ali mwezi Januari mwaka 2011 na uchaguzi kufanyika baadaye mwaka huo. Klay anasemekana kuambia mahakama kuwa wimbo wao unakosoa hali ya sasa serikalini na kote nchini Tunisia tu. Alisema yeye ni mmoja wa wanamuziki wanaokosoa sana serikali na ndio maana wamekuwa wakimsaka sana. Lakini majaji walikataa rufaa aliyowasilisa na kusema hukumu yake ya miezi sita gerezani inastahili kuanza mara moja. Wakili wake alisema kuwa watawasilisha rufaa nyingine kupinga hukumu dhidi yake.

No comments:

Post a Comment