Friday, September 27, 2013

Walioshambulia Westgate Walitoroka Mapema

MAOFISA Usalama wa nchi za Magharibi wanahofia kuwa huenda watekaji wengi waliokuwa wakishikilia kituo cha biashara cha Westgate, walitoroka muda mfupi baada ya shambulio, kwa kutupa bunduki zao na kujifanya wateja wa duka hilo, imefahamika. Mpaka sasa Polisi Kenya inashikilia washukiwa 11 wa ugaidi, akiwamo Mwingereza mwenye umri wa miaka 35 ambaye alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumatatu akijaribu kuondoka nchini humo kwa ndege ya Shirika la Uturuki. Mtu huyo mzaliwa wa kitongoji kimoja jijini Mogadishu, Somalia na aliyepewa hati ya kusafiria ya Uingereza Mei 2011 na kupewa hifadhi ya kisiasa nchini Kenya, alikamatwa na maofisa Uhamiaji baada ya kugundulika kuwa na jeraha usoni na mwilini. Ingawa alikuwa na viza ya Kenya, maofisa hao hawakuwa na kumbukumbu ya kuingia kwake nchini humo. Mpaka jana alikuwa akiendelea kuhojiwa baada ya kudai kuwa majeraha yake yalitokana na mapigano nchini Somalia. Mwanamke aumiza vichwa Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, Joseph ole Lenku alisema juzi kwamba wachunguzi walikuwa wakiendelea kufanyia kazi taarifa kuwa mwanamke Samantha Lewthwaite alikuwa mmoja wa magaidi walioteka Westgate. Alisema: “Katika taarifa zetu za awali tulieleza kutokuwapo dalili zozote zikionesha kuwapo gaidi mwanamke lakini jinsi tunavyoendelea tumeanza kusikia uwezekano huo kuwapo.” Shaka kwamba Mwingereza huyo yawezekana alishiriki ziliongezeka baada ya taarifa ya gazeti la Star jijini Nairobi kukariri manusura wakisema kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akitoa amri kwa magaidi kushambulia. Mmoja alisema: “Mwanamke huyo hakuwa na silaha lakini kila alipotoa amri wanaume walifyatua silaha na kuua.” Poorvi Jain (12), ambaye alishuhudia mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa akiuawa aliwambia walimu wake juu ya gaidi mmoja kuwa mwanamke mweupe, aliyekuwa akifuatana na vijana wawili wa kiume waliokuwa wakifyatua risasi ovyo wakilenga watu waliokuwa ndani ya duka hilo. Al Shabaab ilisisitiza kwamba wageni ndio hasa walikuwa walengwa wa shambulio hilo na kuthibitisha kuwa washambuliaji hao kwa makusudi walilenga Waislamu na wasio Waislamu. Wanamgambo hao walilenga wasio Waislamu na takribani wageni 18 waliuawa, wakiwamo Waingereza na raia kutoka Ufaransa, Canada, Uholanzi, Australia, Peru, India, Ghana, Afrika Kusini na China. Wamarekani watano ni miongoni mwa majeruhi. Lewthwaite anatafutwa akihusishwa na kinachodaiwa ni mipango ya kushambulia hoteli za kifahari na migahawa nchini Kenya. Mipango ya kushambulia hoteli za Mombasa inasemekana kufanana kabisa na iliyofanywa dhidi ya Westgate, ambayo inaripotiwa kupangwa wiki au miezi kadhaa katika ardhi ya Somalia na Al Shabaab. Inaaminika kwamba wapiganaji wa kigeni wanaozungumza Kingereza ndio walichaguliwa kwa umakini mkubwa huku mipango ya kuhujumu Westgate ikipangwa pia kwa uangalifu mkubwa. Timu ya magaidi hao iliingia nchini kupitia mipaka ya Kenya, ambayo mara kwa mara imekuwa ikifanyiwa doria na askari ambao wanalipwa mishahara duni na walinzi ambao ni wala rushwa. Wapiganaji wa Kisomali wanasema hawajapata kutumia magaidi wa kike, licha ya kuwapo hisia za kuhusika kwa Mwingereza Lewthwaite. Wakodi chumba dukani Inadaiwa wapiganaji hao walikodi duka la nguo za kike katika jengo hilo siku moja au mbili kabla ya shambulizi hilo, na kutumia wakati huo kuingiza dukani humo bunduki na risasi za kutosha. Baadhi ya wapiganaji inasemekana walikuwa na mavazi ya kutosha kubadilisha na kujichanganya na raia walikuwa na hofu wakikimbia mashambulizi hayo. Wakati magaidi saba wakiendelea kushikilia mateka kadhaa ndani ya jengo hilo, askari maalumu 20 wa Jeshi la Kenya waliingia kukabiliana nao huku mdunguaji mmoja akihimili askari hao kwa saa 24 akiwa ghorofa ya tatu kabla ya askari hao kudhibiti jengo hilo ilipotimia saa 11.45 Jumanne. Askari wa Kenya baada ya kuingia ndani walizima taa na kamera za CCTV walizokuwa wakitumia magaidi hao na kumudu kuwapiga risasi magaidi waliosalia. Mmoja wao alijilipua. Juzi usiku al Shabaab ilidai kuua watu 50 katika shambulizi la klabu ya usiku mjini Wajir umbali wa maili 70 kutoka jijini Nairobi. Lakini Serikali ilisema waliouawa ni watu watatu tu. Apigwa risasi akiokoa mtoto Wakati huo huo, ilifahamika juzi kwamba baba mmoja alipigwa risasi na magaidi hao wakati akimzuia mtoto wa miaka minne asiuawe katika shambulizi hilo la Westgate. Baba huyo Simon Belcher, ambaye alijisomesha Uingereza, alikuwa amejificha chini ya gari na mkewe na mtoto huyo ambaye hawakuwa na uhusiano naye, pale majeshi ya Kenya yalipoanza kujibu mapigo dhidi ya wapiganaji wa al Shabaab. Wakati magaidi hao wakikwepa mashambulizi ya bunduki, waliwaona watu hao na kumpiga risasi Belcher. Risasi zilimpata begani na kifuani, lakini kwa bahati hazikumpata sehemu muhimu za mwili. Belcher , ambaye ni Mkenya anayeendesha kampuni ya utalii, kutokea nyumbani kwake Nairobi, amelazwa hospitalini na mkewe akimuuguza. Mkewe aliandika kwenye ukurasa wa Facebook kwamba walikuwa na bahati. Waingereza 10 Hadi juzi idadi ya Waingereza wanaoaminika kupoteza maisha katika shambulio hilo ilikuwa ikitarajiwa kuongezeka hadi 10 kutokana na makadirio yanayotolewa na magaidi hao ya jumla ya watu 137 kuwa ndio waliopoteza maisha. Sita mpaka jana ndio walikuwa wamethibitika kufa lakini wachunguzi wanaamini miili ya Waingereza wengine wanne inaweza kuwa imekwama katika kuifusi cha jengo hilo baada ya sehemu yake kuporomoka. Wachunguzi wa Scotland Yard walikuwa wa mwanzo kuingia katika jengo hilo juzi wakitaka kutambua Waingereza hao na magaidi. Askofu aombea magaidi Katika hali isiyotarajiwa, Askofu Mkuu wa Canterbury amekumbwa na lawama baada ya kudaiwa kuwataka waumini wake wasisahau kuwataja watekaji hao katika maombi yao. Askofu Mkuu Justin Welby alitaka Wakristo wote duniani kuombea magaidi walioua watu wapatao 67 jijini Nairobi, Kenya. Welby aliwaambia waumini wasisahau kuombea watekaji hao katika maombi yao, kwa kuwa hata yeye anaombea pande zote; watekaji na watekwaji na waliopoteza maisha na kujeruhiwa na kusema kufanya hivyo kunaendana na mafundisho ya Yesu Kristo. Akihojiwa na BBC juzi, Askofu Mkuu alisema: “Kama Wakristo moja ya vitu ambavyo tunaombea ni haki na hususan masuala yanayohusu hasira ambayo huibuka pale kitu kama hiki kinapojitokeza, lakini tunatakiwa kufanya kama alivyofanya Yesu msalabani alipoombea waliomkosea.” Kauli hiyo imekuja siku mbili baada ya kuandika katika blogu yake kuwa amewaombea magaidi hao. “Leo naombea wote wanaoendelea kushikiliwa na watekaji katika kituo cha biashara Nairobi, pia familia zao na marafiki wanaosubiri kwa hamu kusikia mustakabali wao,” aliandika. “Naombea pia watekaji wao, kwamba waweze kuona na kuelewa kwamba uadui na ghasia havitaruhusiwa kutawala.” Askofu Mkuu Welby aliendelea kusema kuwa waathirika wa shambulio dhidi ya kanisa nchini Pakistan wanapaswa kuchukuliwa kama mashahidi wa Ukristo. Watu wapatao 80 waliuawa katika mashambulizi mawili katika Kanisa la Watakatifu Wote jijini Peshawar wakati waumini wakiondoka kwenye Misa ya Jumapili. Askofu Mkuu Welby ambaye anaongoza Kanisa la Anglikana duniani, alisema waathirika wa mashambulizi hayo walilengwa kwa sababu ya imani yao, na kutaka Serikali ya Pakistan kufanya iwezalo kulinda raia wake. “Nadhani Wakristo wanashambuliwa katika matukio kadhaa kwa sababu tu ya imani yao,” alisema. “Nadhani ni kweli kusema kwamba katika Kanisa la Watakatifu Wote tumeshuhudia zaidi ya mashahidi 80 katika siku chache zilizopita. “Wameshambuliwa kwa sababu walikuwa wakithibitisha imani yao katika Yesu Kristo kwa kwenda kanisani na kwamba hiyo haiwezi kukubalika katika mazingira yoyote kwa sababu yoyote ya tofauti za kidini.” Filamu ya kutisha Vikosi vya Kenya vilisema ndani ya jengo hilo kulionekana sawa na ‘filamu ya kutisha’ kutokana na kutapakaa kwa damu kila mahali na miili iliyosambaa katika sakafu. Idadi rasmi ya Serikali ya watu waliokufa ni 67- raia wakiwa 61 na maofisa wa usalama sita – na Kikosi cha Msalaba Mwekundu kina orodha ya watu 63 ambao haijulikani waliko. Al Shabaab inashikilia kuwa imeua watu 137.

No comments:

Post a Comment