Friday, September 27, 2013

Rais Kikwete Kuifumua TANESCO

RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali yake inafanya mageuzi muhimu na marekebisho makubwa katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa nia ya kuharakisha jitihada za Serikali kusambaza umeme kwa wananchi wengi zaidi. Pia, amesema Serikali imechukua hatua nyingi na kali za kupambana na rushwa, kwa nia ya kukomesha vitendo hivyo nchini na kuinua kiwango cha utawala bora. Alisema hayo juzi wakati alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Daniel Yohannes. Ujumbe huo umekutana na Rais Kikwete, New York, Marekani ambako Rais amefikia kwa ziara yake ya kikazi, ambako miongoni mwa mambo mengine, atahutubia mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), ulioanza Jumanne wiki hii. Katika mazungumzo hayo, Yohannes alimwelezea Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ombi la Tanzania kuingizwa katika awamu ya pili ya misaada ya Serikali ya Marekani kupitia MCC, chini ya Akaunti ya Milenia Tanzania (MCAT). Nchi nyingine za Afrika ambazo maombi yao yanafikiriwa katika awamu hiyo ya pili ni Morocco, Mozambique na Lesotho. Tanzania ndiyo nchi iliyopokea sehemu kubwa zaidi ya msaada wa MCC duniani katika awamu ya kwanza, ambako ilipewa kiasi cha dola za Marekani milioni 698 ambazo zimeingizwa katika miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme vijijini, miradi ya maji na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia. Serikali ya Tanzania imeamua kuwa fedha za awamu ya pili ya MCC zitaingizwa kupanua zaidi huduma za umeme na ujenzi wa barabara za vijiji kwa nia ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata huduma za umeme na kwa nia ya kuboresha barabara za vijijini katika maeneo yanayozalisha mazao kwa wingi zaidi. Serikali ya Rais Kikwete imeliweka suala la usambazaji umeme kwa Watanzania mijini na vijijini miongoni mwa maeneo yake ya kipaumbele. Wakati anaingia madarakani mwaka 2005, ni asilimia 10 tu ya Watanzania waliokuwa wanapata umeme. Katika miaka saba iliyopita, asilimia hiyo imepata hadi kufikia 21 ikiwa ni asilimia 11 zaidi kuliko katika miaka yote 50 ya Uhuru. Lengo la sasa ni kuifikisha asilimia 30 ama zaidi mwaka 2015. Katika mazungumzo hayo na Rais Kikwete, Yohannes alitaka kujua ni hatua zipi Serikali inazichukua kurekebisha changamoto zinazoikabili TANESCO na hatua gani zinachukuliwa kuzidi kukabiliana na matatizo ya rushwa. Rais Kikwete amemweleza Yohannes: “Kama unavyojua, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepitia safari ngumu na kukabiliwa na changamoto nyingi lakini sasa tumeamua katika Serikali kulifanyia mageuzi muhimu na marekebisho makubwa kwa maana ya muundo wake na pia kuangalia viwango vya malipo ambayo Shirika hilo linawatoza wateja wake. Mageuzi haya katika TANESCO ni muhimu sana na yameanza kufanyika na kwa hakika Serikali imedhamiria kukayamilisha mageuzi hayo katika muda mfupi iwezekanavyo.”

No comments:

Post a Comment