Saturday, September 28, 2013
Shujaa Hajji
Mwanamke Mmarekani mama wa watoto watatu aishiye Nairobi siku ya tukio aliondoka nyumbani na familia yake na kwenda katika duka hilo na kujikuta amenaswa katika shambulizi hilo akiwa na mabinti zake watatu.
Katherine Walton, ambaye alikuwa Afrika akifuatana na wanawe na mumewe Phillip, tangu miaka miwili iliyopita, alijikuta amenasa chini ya meza nje ya duka hilo. Anasema kama asingekuwa mwanamume aitwaye Abdul Haji, hana uhakika kama yeye au wanawake na watoto aliokuwa amenasa nao kwa saa kadhaa, wangetoka wazima. Familia ya Walton ilielezea mkasa huo kwa Telegraph la Uingereza ikifafanua kilichojiri na hata Haji kuonekana akiwaokoa huku milio ya risasi ikirindima na miili yenye damu ikionekana kila mahali.
“Tulikuwa tukienda kuonana na wanangu wawili wakubwa wa kiume katika duka hilo tuliposikia mlipuko,” Walton (38), ambaye aliingia Kenya akitoka North Carolina, aliiambia Telegraph.
“Niliwashika mabinti wale na kuanza kukimbia. Mwanamke alituvuta nyuma ya meza. Niliweza kuona risasi zikigonga juu ya maduka na kusikia vilio katika sehemu tuliyokuwa.”
Walton na wanawe walinasa pamoja na mwanamke Mkenya na wanawake wawili Wahindi chini ya meza kwa saa kadhaa. Wanawake wengine walimsaidia Walton kutuliza mabinti zake.
“Walionekana kutulia kimya,” Walton alisema.
“Mwanangu alikuwa akilia huku milio ya risasi ikiendelea, baadaye alilala. Wakati fulani mapambano yakiendelea, mwanangu wa miaka miwili na mtoto mwingine walikuwa wakichezea simu yangu.
Sikuwaelewa kufanya vile kana kwamba mambo yalikuwa mazuri.”
Baada ya kilichoonekana sasa kama mvumo wa risasi huku vilio vya magaidi na waathirika vikichangia, Walton ghafla aliona mtu akiwa na bastola akijibu mashambulizi ya magaidi hao.
Alikuwa ni Haji, mtu ambaye alipata mafunzo ya kivita na baba yake ambaye alipata kuwa Waziri wa Usalama, na alikuwa akijaribu kuelekeza wanawake wamfuate. Mtoto ajitokeza Walipokuwa wanahofia kutembea kama kundi, mwanawe mwenye umri wa miaka minne, Portia ambaye alijitokeza chini ya meza alimfuata Haji.
“Sijui alijuaje kufanya hivyo lakini alifanya,” Walton aliiambia Telegraph.
“Alifanya alichoambiwa kufanya na alikwenda.” Picha za Portia na Haji zilisambazwa katika mitandao mingi na zingine zikimwonesha Haji akiokoa wanawake na watoto.
Walton alifarijika kubaini kuwa wanawe wa kiume aliokuwa akutane nao dukani pale walikuwa salama nyuma ya mstari wa Polisi nje ya duka. Walton aliiambia Telegraph:
“Nilikuwa nahofia familia Marekani kuona picha hii, kwa sababu sijawasilimulia lolote kuhusu tukio kamili. Kwangu mimi najua habari yote kwa undani na kwamba ilimalizika salama. Nadhani Haji ananidai fadhila.”
Haji alipoulizwa kuhusu ujasiri wake, alisema :”Nadhani nimefanya kile ambacho Mkenya yeyote katika hali kama ile angeweza kufanya kuokoa maisha, kuokoa binadamu wengine bila kuangalia uraia, dini au imani.”
Mashuhuda wa tukio hilo waliiambia AP na vyombo vingine vya habari, kwamba magaidi walizingira wateja na kuwauliza juu ya Uislamu na kwamba Mwislamu anapaswa kuufahamu na kuwataka Waislamu kuondoka. Lakini bado baadhi ya Waislamu walikuwa miongoni mwa waliouawa. Al Shabaab ilipoulizwa kama nia yao ilikuwa kuua wageni, ilisema:
“lengo letu lilikuwa ni kuishambulia Serikali ya Kenya katika ardhi yake na eneo lolote ndani ya Kenya ni lengo letu halali … na Kenya inapaswa kuwajibishwa kwa hasara hiyo ya maisha, yawe ya mgeni au mwenyeji.”
Akihojiwa na NTV, Haji alikiri kwamba kaka yake – aliyempeleka kwa mara ya kwanza kuokoa katika duka hilo – ni mpambanaji dhidi ya ugaidi na hadi shambulizi linatokea alikuwa akiifanya kazi hiyo kwa siri.
Alisema wao na baba yao walipokea vitisho dhidi ya maisha yao siku moja kabla ya shambulio hilo na sasa ni dhahiri kwamba kaka yake alikuwa akifanya kazi ya kupambana na makundi kama al Shabaab.
Kiongozi wa al Shabaab, Ahmed Godane, alisema katika taarifa yake Jumatano kwa njia ya redio, kwamba shambulizi hilo lilifanyika ili kulipiza kiasi kwa mataifa ya Magharibi yanayounga mkono uvamizi wa Kenya nchini Somalia na ‘maslahi ya kampuni zao za mafuta’.
Ingawa Kenya kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje mapema ilisema raia wawili au watatu wa Marekani walihusika na shambulio hilo, ofisa wa mataifa hayo alisema baada ya kuchunguza pasipoti na kumbukumbu za wakimbizi, hakuna ishara yoyote inayothibitisha Wamarekani kushiriki.
Majiji kadhaa ya Marekani hususan Minneapolis, yana jamii nyingi za Wamerakani wenye asili ya Somalia. Magaidi Jumatano waliendeleza mashambulizi mengine safari hii wakishambulia mji wa Wajir, katika mpaka na Somalia ambako inaarifiwa mtu mmoja aliuawa na wengine wanne kujeruhiwa, baada ya mtu mwenye silaha kuwafyatulia risasi na kuwarushia mabomu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilisema.
Maofisa wa mochari jijini Nairobi wamejiandaa kupokea idadi kubwa ya miili ambayo bado imo dukani. Maofisa wa Serikali waliiambia AP kwamba kituo hicho cha biashara, bado kinaweza kuwa na idadi kubwa ya miili. Serikali imethibitisha jumla ya vifo 72: raia wakiwa 61, maofisa usalama sita na magaidi watano. Chama cha Msalaba Mwekundu kinasema watu 71 haijulikani waliko.
Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec alisema Jumatano kwamba nchi yake inatoa msaada wa kiufundi na vifaa kwa vikosi vya usalama vya Kenya na wahudumu wa afya.
Godec alisema Marekani inasaidia uchunguzi ili hatimaye kupata magaidi waliohusika na kuwafikisha mbele ya sheria. Maofisa wa Serikali ya Kenya wamesema washukiwa 11 wanashikiliwa wakiwamo saba ambao walikamatwa katika uwanja wa ndege wakijiandaa kuondoka.
Wanahojiwa, alisema msemaji wa Serikali. JK atoa pole ubalozini Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete jana alitembelea Ubalozi wa Kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa(UN), New York, Marekani na kusaini kitabu cha maombolezo kutokana na vifo vya watu 69 na mamia kujeruhiwa katika shambulio hilo.
Rais aliwasili ubalozini hapo saa 8:30 mchana baada ya kutembea kwa miguu na walinzi wake kutoka makao makuu ya UN karibu na ubalozini hapo na kupokewa na Balozi Koki Muli Grignon, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika UN kwa niaba ya Balozi Macharia Kamau ambaye yuko nje ya Marekani.
Baada ya kusaini, Rais alizungumza kwa ufupi na wafanyakazi wa ubalozi huo, akisema alikwenda kuelezea majonzi na hasira yake kutokana na vifo vya watu hao na mamia wengine kujeruhiwa.
“Siku ile ya tukio nilikuwa natoka Canada kuja hapa na nililiona kwenye televisheni, nikiwa Canada. Nilimpigia simu Rais Uhuru Kenyatta na kuzungumza naye. Nilimweleza masikitiko yangu na hasira yangu kwa shambulio hilo dhidi ya watu wasiokuwa na hatia na raia wasiokuwa na ujuzi wowote wa kupigana,” Rais Kikwete alisema na kuongeza:
“Nilimweleza utangamano wa Watanzania na Wakenya katika tukio hilo. Nilimwambia kuwa wananchi wa nchi zote mbili wako pamoja katika kipindi hiki kigumu, ni majirani na watu wale wale. Nilimwambia kuwa tutaendelea kushirikiana kupambana na ugaidi kwa sababu wakati wa tukio la Septemba 1998, Nairobi na Dar es Salaam wote waliathirika.
“Nilimwambia Tanzania iko tayari kusaidia kuchangia mawazo na rasilimali kutafuta suluhisho la tukio hili kama msaada wetu ungehitajika. Nilimtakia yeye na wananchi wa Kenya moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.” Balozi Koki Muli Grignon amlimwambia Rais Kikwete:
“Umetupa heshima kubwa kuja hapa, umetupa hamasa na ari. Tutapambana pamoja kukomesha ugaidi katika eneo letu la Afrika Mashariki.
Ujio wako umetushangaza, umemshangaza kila mtu kwenye ubalozi. Hatukutarajia kabisa. Tunakushukuru Rais.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment